KIKUNDI KINACHOTETEA WANAOUGUA UKIMWI




KIKUNDI KINACHOTETEA DHULUMA ZA WANAOUGUA UKIMWI

Madhila ambayo anayapitia mtu aliye na virusi vya HIV ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Ukimwi bado ni mengi mno.Ingawa kumekuwa na kampeini kali za kuwahamasisha watu na kuwapa ufahamu ili wasiwatenge watu wanaougua ugonjwa huu,yamkini juhudi hizi zimekuwa bure bilashi huku jamii ikizama katika lindi zito la kupuuza athari anazopata mtu anayeugua ugonjwa huu.

Hivi majuzi mahakama moja jijini Nairobi ilitoa uamuzi wa kihistoria pale ilipomtaka mfanyikazi mmoja ambaye alipimwa virusi bila hiari yake na hatimaye kufutwa kazi na muajiri wake kulipwa kwa dhuluma aliyofanyiwa.

Uamuzi huu ulipokolewa vyema na Wakenya ambao wamekuwa wakiendeleza kampeni za kuwalinda vyema na kuwachukulia wagonjwa wa ukimwi kama watu ambao mchango wao katika jamii bado unahitajika sana.

Na juhudi hizi hazijaishia tu kwa mashirika au makundi makubwa ya haki za kibinadamu,vijijini ujumbe huu umekuwa ukiendelezwa bayana huku watu wakitakiwa kutowabagua wale wenye virusi katika jamii.Kwa sababu ya kutokuwa na sheria mwafaka ambazo zingelifaaa kuwalinda wale wanaopatikana na virusi hivi vya Ukimwi,baadhi yao hubaki wakiachishwa kazi na wengine hata kufungiwa majumbani,mbali na majuto tele ambayo wanayapitia kimya kimya.

Lakini kikundi kimoja katika lokesheni ya Matsangoni kimeamua kuweka bayana kampeini zake kuhusu madhila ambayo wanaopitia wale wote wenye virusi vya ukimwi.Kikundi hiki kilikuwa mojawapo ya vikundi ambavyo viliigiza kwa ustadi katika mchezo wao uitwao ukimwi katika shule ya msingi ya Matsangoni.

Kwenye mchezo huo ambao uliwaacha wengi wakiwa wameduwaa kutokana na usanifu wa hali ya juu,kijana Faraj(Fiesta Lewa) anampenda msichana kwa jina Pendo(Santa Julius) na wote wanapeleka habari hizo kwa wazazi wao.Wazazi wa Pendo,Victor Gari Mwanyonyo na Magret Nyamvula wanamtaka binti yao amlazimishe mpenzi wake Faraja waende wakapimwe HIV kabla ya ndoa yao.

Hilo pia linafanyika katika nyumba ya akina Faraj ambao wazazi wake(Janet Tido na Kelvin Deche) wanataka pia kijana wao na mpenziwe wakapimwe ili wajue hali zao za kiafya.Pindi tu wanapopimwa,Pendo anapatikana hana virusi lakini kiosha roho wake(Faraj) anajipata kaathirika na ugonjwa.

Hapo kasheshe inaanza kutawala huku wazazi wa pande zote mbili wakikorogana vikali wakitaka ndoa hiyo isifanyike.Baya zaidi bosi wa Faraj kule akaofanyia kazi(Rodgers WAgure anapata habari kuwa Faraj ana ukimwi na bila kusita anaamua kumfuta kazi.Hili pia linaathiri uhusiano wa bosi na binti yake(Priska Mapenzi) ambaye anahoji ni kwanini babake akamfuta kazi Faraj.Mzozo unakuwa mkubwa hivi kwamba anahitajika mshauri wa pande zote mbili pamoja na bosi huyo.Hapa anafika Mjomba Agustus ambaye kwa juhudi kubwa anaamua kutoa ushauri na hali inabadilika kabisa.Familia zote mbili zinaamua kuwa lazima Faraj apewe matumaini na kwamba kupata ukimwi sio mwisho wa maisha na kwamba bado anaweza kuendeleza na mipango yake ya baadaye.

Hilo linafanyika na amani kote huku wakiwa mbele ya jukwaa la wageni wanaamua kushikana mikono na kwa hilo umati akiwemo mkuu wa wilaya ya Kilifi na DO wa Bahari Florence Sitawa unaachwa ukiwa na furaha.

Baadaye Taifa Leo iliweza kuongea na msemaji wa kikundi hiki Bw.Victor Gari ambaye alisema kikundi cha Tabasamu Youth Association kinajishughulisha na kuelimisha wanakijiji kuhusu masuala mbalimbali ya ufahamu ambayo ni ndara kufika vijijini.”Sisi huwa pia ni washauri rika na hutumia muda mwingi kufika vijijini na kutoa ushauri kuhusu elimu ya kijamii,vita dhidi ya ugonjwa wa ukimwi na pia kuhusu mamba za mapema na kikwazo chake katika maisha ya kila siku.” Akasema.

Naye mwelekezi wa mchezo huo,Fiesta Lewa ambaye anacheza kama Faraj alieleza matumaini yake kuwa angaa wamefanikiwa kugeuza hali ya maisha ya watu wa Matsangoni kwa kutoa ushauri kuhusu masuala mbalimbali ya elimu ya kijamii.”Unakuta kwamba mbali na michezo hii,sisi tumeona haja kubwa ya kuelimisha umma na hasa katika ndani vijijini ambapo elimu ya jamii imepuuzwa na kukosa mwelekeo hitajika.” Akasema.

Alisema kikundi hiki kina zaidi ya wanachama 25 na kwamba wao huwa na kila aina ya michezo inayoendana na mazingira ya halfa yenyewe.”Sisi kama kikundi cha kutumbuiza na kuelimisha huwa tuna hazina kubwa ya michezo,nyimbo na mashairi ambayo huwa tuko tayari kuyatoa kwa umma kutusikiliza kwa vile tunaamini nia katika mihadhara hii ambapo ujumbe huu unafika ndani kabisa kijijini.” Akasema Gari.

Kuhusu mchezo huu wao,GAri alisema waliutunga ili kuelezea kwa kina vile mtu mwenye ukimwi huteseka lakini pia vile jamii inaweza kugeuza hali ikiwa kutakuwa na ushirikiano mwema.”Hii ndio sanaa na ni moja ya kazi zetu za kuelimisha jamii.”akasema akiongea na Taifa Leo katika shule hiyo.

Comments