JUHUDI ZA KUTUNZA MAZINGIRA KATIKA MAENEO KAME NCHINI KENYA.







JUHUDI ZA KUTUNZA MAZINGIRA KATIKA MAENEO KAME.




(Badala ya kuchoma makaa,sasa wakazi washauriwa wafuge kanga na kuuza)

Hivi majuzi,waziri wa mazingira Bw.John Michuki alitangaza mikakati mipya ya kutunza mazingira hasa katika juhudi za uboreshaji wa misitu ya humu nchini ambayo katika siku za hivi karibuni imekuwa walengwa wakuu katika uharibifu wa mazingira unaoendelea katika kima cha kutisha.

Na huku mgogoro kuhusu ukataji miti na shughuli za kilimo ukiendelea kutoa tumbo joto katika msitu wa Mau huko Riftvalley,kampeini za aina yake za kutunza mazingira kwa hivi sasa pia zimeanzishwa katika maeneo kame.

Na kama vile Taifa Leo ilivyogundua ilipokuwa katika eneo la Bachuma Gate huko Voi hivi majuzi,sasa juhudi za kutunza mazingira zimeingiliwa na wakazi wanaotaka kuhakikisha kwamba misitu inalindwa.

Waziri Michuki akiongea hivi majuzi alisema wizara inatayarisha sera ambapo kila mkulima atatikana kutumia asilimia kumi ya shamba lake katika upanzi wa miti.Hii waziri alisema itasaidia pakubwa katika kuhakikisha Kenya inabakia kuwa na mazingira mema baada ya kuona athari za kukatwa kwa msitu wa Mau zikianza kuathiri wakenya.

Katika eneo la Bachuma,Mzee Gerald Macharia mtaalam wa mazingira katika maeneo kame pamoja na Joseph Mburu wameanzisha maradi wa aina yake ambao watarajia kuwa utapunguza kwa kiasi kikubwa shughuli za uchomaji makaa na ukataji kuni katika maeneo haya ambayo ni kame na hupata mvua chache kwa mwaka.

Katika maeneo haya ambayo yanapakana na Samburu,Makina na Maungu,shughuli za ukataji miti zimekuwa zikiendelea kwa kiwango cha kutisha na kutoa taaswira ya kuendelea kwa jangwa katika maeneo haya.

Ni kawaida mtu anapopita katika maeneo haya hasa anaposafiri kwenye barabara kuu itokayo Nairobi kuelekea Mombasa ataona wauzaji makaa kando mwa barabara wakinadi bidhaa hiyo.

Lakini kulingana na Mabw.Macharia na Joseph Mburu,wao wameanzisha kampeini za kuhakikisha kuwa wakazi wanaacha kabisa masuala ya kukata miti na kuchoma makaa badala yake wanawafunza jinsi ya kufuga kanga na kuuzia watalii katika eneo hilo.

Huku wakishirikiana sako kwa bako na shirika la hifadhi ya wanyama pori nchini(KWS) Bw.Mburu na Bw.Macharia wamekuwa wakiingia kutoka kijiji kimoja hadi chengine kuwaelimisha wakazi juu ya mpango huu.”Badala ya wao kukata misitu na kuharibu mazingira,sisi tumeanzisha kampeini za kuwahimiza wafuge kanga na kuwauza kwa watalii na mahoteli katika miji ya Nairobi na Mombasa ambapo wanaweza kupata fedha nyingi na wakaendeleza maisha yao,” akasema Bw.Mburu.

Wakiongea na Taifa Leo katika eneo ambalo wanafugia kanga wengi katika kituo kidogo cha biashara cha Bachuma,mkabala na hoteli ya Tsavo Mashariki,wawili hao walisema kampeini yao imeanza kuzaa matunda kwani baadhi ya wakazi wameanza kuingia mradi huu na pole pole wameamua kuacha kuchoma makaa na wanafuga ndege hawa kwa wingi na kujipatia pato la kila siku.

Katika kituo chao ambacho kimesajiliwa na kutambuliwa na shirika la kuhifadhi wanyama pori(KWS),Macharia na Bw.Mburu wamekuwa wakifuga kanga wengi pamoja na wanyama wengine wa mwitu kama vile sungura.

Katika maeneo kame,maisha huwa ya taabu kwani bayana njaa huonekana kuandama wakazi kila mara.Na kwa kutafuta pesa za haraka,wakazi hukata miti na kuchoma makaa na kuuza kuni katika harakati za kujipatia riziki.

Hiyo ndiyo changamoto ambayo Macharia na Bw.Mburu waliangalia kwa makini na kuona kuwa njia mbadala ya kuhifadhi miti michache iliyopo katika maeneo haya ni kupitia kwa mpango huu.

“Katika nyakati za kwanza hali ilikuwa ngumu na watu wengi walichukulia kimzaha mwito huu lakini walivyoona wanaweza kufuga kanga na kuuza na kupata pesa,sasa wakaamua kujaribu na wengine tayari wameanza kuuza ndege hawa katika hoteli zilizoko katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

Wakati Taifa Leo ikiwasili katika mradi huo wa Game Rescue Foundation,Bw.Mburu na Mzee Macharia walikuwa wamewasili muda mchache kutoka Taru ambapo walikuwa na warsha ya siku moja kuwaelezea wakazi kuhusu mradi huu ambao pindi ukishika kasi,biashara ya makaa na uharibifu mwengine wa misitu itapungua au kumalizika kabisa.

Miezi miwili iliyopita,Bw.Mburu na Macharia walikuwa katika eneo la Maji ya Chumvi ambapo walikuwa na warsha nyengine ya kuwahamisha wakazi waache kuchoma makaa lakini badala yake waanze kufunga kanga ili wauze na kupata mapato.

“Tunafahamu kuwa hali ya maisha katika maeneo kame daima imekuwa ngumu lakini pia tumewaeleza wakazi juu ya mchango mkubwa ambao wanatakikana wawe nao katika kufanikisha mazingira yao,” akasema Bw.Mburu.

Kwenye kituo chao(Sanctuary) wamekuwa wakifuga aina mbili za kanga wajulikanao kama Helmeted guinea fowl na vultureline guinea fowl.”Hawa ndio wanaopatikana katika maeneo kama kama haya lakini kuna ile aina ya kanga aitwaye christened guinea fowl ambaye hupatikana tu katika maeneo yenye misitu mikubwa na baridi kali.

Kulingana na kifungu 376 cha sheria za kuhifadhi na kusimamia wanyama wa pori,kanga wanaruhusiwa kunaswa katika msimu unaoanzia mwezi wa machi hadi mwezi wa novemba.Miezi ambayo KWS inapiga marufuku unasaji wa kanga ni kuanzia mwezi wa desemba hadi feburari.

Kulingana na Bw.Mburu,mradi huu huenda ukawa na faida kubwa kwa wakazi wa Bachuma na viunga vyake kwani mbali na kuwa wakazi sasa wanaanza kupata ajira,hapa sasa kutatumika kama kituo ambapo habari muhimu kuhusu wanyama pori zinaweza kupatikana hasa kwa wasomi na wanasayansi.

“Hiki ni kituo ambacho tunataka kiwe kielelezo kuwa hata katika maeneo kame kama haya juhudi za kuhakikisha mazingira bora na maisha mema zinaweza kuafikiwa,” akasema Mzee Macharia.Kwa sasa wao wana takribani kanga 60 ambao wanafuga na juzi walipata oda inayowahitaji kusafirisha kanga 300 hadi nchini China.

Kutokana na eneo hili kupata mvua chache sana kwa mwaka,wakazi wengi huwa wafugaji ingawa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo njaa isiyo na kikomo.Hali hiyo huwafanya wengi wao kubakia kula matunda ya mwitu kila msimu.

Akiongea na Taifa Leo katika eneo la Makina,mmoja wa wakazi ambao waliamua kuacha kuchoma makaa na badala yake ameanza kufuga kanga Bw.Joseph Mwero alisema anatarajia kuanza maisha mapya katika biashara hii ya kufuga kanga.

”Kwanza biashara yenyewe ilikuwa imeingiliwa na watu wengi hivi kwamba ilikuwa hata kuuza gunia moja la makaa ni tatizo;Lakini tulipoenda kwa semina hii huko Taru,niliamua sitokata tena makaa na badala yake nitajitahidi kufuga ndege hawa kama njia badala ya kuendeleza maisha yangu,” akasema.

Maoni yake yalikuwa sawia na yale ya Justine Mkalla ambaye tulikumbana naye katika eneo la Maji ya Chumvi tukirudi jijini Mombasa.Yeye pia aliniambia kwamba ameamua kuacha mambo ya kuchoma makaa na badala yake ameamua kuanza kufuga ndege hao ili apate kuwauza na kuendeleza maisha yake.

Wakati Taifa Leo ikiondoka katika eneo hilo,sura ya matumaini ilikuwa bayana kwani sasa wakazi wameona mwanga na wanaapa kushirikiana na KWS pamoja na mpango huu ili kuhakikisha pia nao wanapata vibali na kufunga ndege hao ambao huwa na soko kubwa nchini na kimataifa.

Comments