Mikoko inafaa kutunzwa kama wafanyavyo hawa vijana wa Majaoni huku Mombasa.





Hapa vijana hawa wanaonekana wakimuonyesha muandishi Lewa Jefwa jinsi wanavyofanya kazi zao katika mradi wao wa kukuza mikoko katika kijiji cha Utange-Majaoni huko Mombasa.

Note:Shukrani zangu kwa Bwana Lewa Jefwa kwa kuniruhusu kutumia habari hii kutoka kwa makala zake anazochangia hapa Mombasa.






Kazungu

WANAPANDA MIKOKO KUTUNZA MAZINGIRA

Kijiji cha Majaoni ni kijiji ambacho kimejificha kwa utulivu katika eneo la Mombasa kaskazini.Kinapatikana karibu na kituo cha biashara cha Shanzu karibu na eneo la Mtwapa.

Hata hivyo mbali na utulivu ambao unakiandama kijiji hiki,kikundi kimoja cha vijana katika sehemu hii kimedhihirisha nia yako kubwa ya kutunza mazingira hususani upanzi wa mikoko.

Hivi majuzi nilibahatika kukutana na vijana hao wakiwa katika shughuli zao za kuwatembeza wageni katika mradi wao ambao sasa umekuwa kielelezo katika sehemu hii ya Majaoni.

Na katika kile kilichoanza tu kama kikundi cha kujaribu kuwaleta pamoja vijana wa Majaoni,sasa kikundi cha Majaoni Youth Development Group kimeanza kuwavutia watafiti wa mazingira kutoka idara tofauti ambao hufika hapa kuelezwa kwa kina na vijana hawa jinsi wanavyotekeleza mradi wao.

Ni kikundi ambacho kilianzishwa mwaka wa 2003 na vijana 11 kutoka mtaa huu wa Majaoni na leo hii juhudi zao za kukuza mazingira bora zimekuwa zikiwavutia watu wengi ambao hufika kila mara katika mradi huu.

Na kwa muda huu wote ambao wamekuwa wakijishughulisha na kazi hii ya upanzi wa mikoko na miti mingine mingi vijijini,wamefaulu kupanda zaidi ya mikoko 30,000 katika ufuo wa huu wa Majaoni.Wao hupanda mikoko kila msimu wa mvua unapokaribia na ni bidii ndiyo ambayo imefanya baadhi ya sehemu ambazo awali zilikuwa zimekatwa miti hii kuwa tena na mikoko.

Wanachama ambao wanaunda kikundi hiki ni Bw.Lucas Fondo ambaye ndiye mwenyekiti wa kikundi hiki,David Taura ambaye ni katibu wa kikundi hiki akisaidiana na Daniel Shida naye Caroline George akiwa mweka hazina wa kikundi hiki.Wanachama wengine ni Kahindi Kazungu,Saumu Iddi,Mboje Idd,Musa Kalama,Morris Ngome,Samuel Deche na Patrick Kivatsi.

Akiongea na Taifa Leo kwenye mradi wao,msemaji wa kikundi hiki David Taura alisema kuwa ingawa wao walianza miradi yao mwaka wa 2003,lengo la kuanzishwa kwa kikundi hiki lilikuwa limeafikiwa mwezi wa Desemba mwaka wa 2002.

”Tuliamua sisi kama vijana katika eneo hili tunahaja ya kuboresha mazingira yetu na jambo la kwanza lililotujia akilini ilikuwa ni kuanza kutunza mikoko hii ambayo ilikuwa ikiangamia kwa wingi kutokana na ukataji kiholela.” Akasema.

Na punde tu baada ya habari zao kuanza kujulikana kijijini,washika dau katika sekta ya mazingira kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na hata idara za serikali zinazohusiana na mzingira wamekuwa wakifika hapa na kujionena jinsi vijana hawa wanavyofanya kampeni kabambe kuhakikisha kuwa mazingira hayaharibiki.”Sisi lengo letu ni kulinda mazingira yetu na jambo hili linaanza kutimia kwa sasa.

Na Je wanakijiji wamechukuliaje juhudi za kikundi hiki kuamua kutunza mazingira na kupinga ukataji ovyo wa mikoko ambao unahatarisha hata samaki na viumbe wengine wa baharini ambao hutegemea mmea huu kama chakula chao?

Taura anasema kuwa ilikuwa kazi ngumu kwani wakazi wengi walikataa mwito wetu wa kutokata mikoko na waliendelea lakini hili halikuwavunja moyo na leo hii wanaendeleza kampeni zao huku baadhi ya wanakijiji wakikubaliana nao.

”Kila kitu kinapoanza huwa vigumu mno kwa sababu wanakijiji hawa hawakutaka kutusikiliza nyakati za mwanzo lakini jinsi tulivyoendeleza na kampeni zetu basi hapo ndipo walipobaini kile tulichokuwa tukiongea.” Akasema

Na juhudi zao za kuwataka wakazi wa Majaoni watunze mazingira kwa kupanda miti hazijaishia tu vijiji,Kahindi Kazungu ambaye ni mmoja wa wanachama wa kikundi hiki amekuwa akizunguka kutoka shule moja hadi nyengine kupeleka ujumbe huu wa kupanda miti.

“Tunalenga hata shule na maeneo mengine ya hadhara kama vile mikutano ambapo ari yetu itafikia wengine na tunashukuru kuwa juhudi hizi sasa zinaelekea kufaulu.” Akasema huku akituonyesha eneo ambalo walipanda mikoko baada ya miti hiyo kukatwa na eneo hilo kubaki bila hata mti mmoja.

”Unaona eneo hili,hii ni mikoko ambayo sisi tulipanda baada ya uharibifu ambao ulikuwa umefanywa awali kwa hivyo hizi ni juhudi ambazo zinafaa kujengwa na kukuzwa.” Akasema Danile Shida ambaye ni naibu katibu katika kikundi hicho.Mwaka huu,kikundi hiki kilipata wageni kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu ambao hufika na kufanya utafiti wa viumbe wa majini katika ufuo huu.

Vile vile shirika la Pwani Christian Community Services(PCCS) ambalo ni kitengo cha kanisa Angilikana dayosisi ya Mombasa liliamua kuwafadhili na kuwapa miche 60,000 ambayo wamekuwa wakitoa kwa wakazi vijijini ili kupanda kama njia mojawapo ya kutuna mazingira.

Si hayo tu,Shirika la Diaknie Emergency Aid liliko jijini Nairobi majuzi liliwatuma watu wake kuja na kuangalia na kujifahamisha kuhusu mradi huu wa kukuza mikoko unaoendelezwa na kikundi hiki.

Wawili hao Dkt.Jane Wamatu na Roland Kilian Schlott walifurahishwa na mradi huu na kuwasifu vijana hao kwa juhudi zao.Vile vile Shirika la East Africa Wildlife Services (EAWLS) limekuwa likiwatuma baadhi ya maafisa wake kuangalia jinsi vijana hawa wanavyofanya kazi ya kutunza mazingira na zile changamoto ambazo wanakumbana nazo wakiwa katika shughuli zao.

Kutokana na bidii yao,wamekuwa kielelezo cha kutolewa mifano hivi kwamba sasa wanatambuliwa na kitengo cha viumbe wa baharini katika shirika la KWS na vile vile idara ya misitu katika wilaya ya Mombasa.

Comments