SHIRIKA LA KUTETEA WANAWAKE KILIFI KUZINDUA KAMPEINI ZAKE

Shirika moja la kutetea haki za wanawake katika kaunti ya Kilifi  limeahidi kuhakikisha kwamba mimba za mapema zinaisha katika eneo hilo.
Shirika hilo la Kilifi Women Network Organization(KIWNET) kupitia kwa mwenyekiti wake Bi Esther Kondo lilisema kuwa kaunti ya Kilifi imeorodhesha visa vingi zaidi vya mimba  za mapema na jambo hilo lazima lishughulikiwe kwa makini zaidi.
"Kila uchao, visa vya mimba za mapema katika kaunti ya Kilifi vimeongezeka maradufu. Ni kwanini basi kama jamii tusiketi chini na kuangalia njia za kukabili tatizo hili.Lazima sasa tufungue macho yetu na kuangalia mbele zaidi," akasema Bi Kondo.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kati ya Januari na Machi mwaka huu, jumla ya wasichana zaidi ya 2,000 wengi wao wakiwa chini ya umri wa kati ya miaka 15-19 ni wajawazito.
"Hatuwezi kuketi chini tukiangalia watoto wetu wakiendelea kutaabika. Lazima kama jamii tujue ni nini tunachofaa kufanya," akasema Bi Kondo.
Kundi hilo lilianzishwa mapema mwaka huu na wanaharakati wa kukabiliana na mimba za mapema baada ya kaunti hiyo kushuhudia visa hivyo kwa kiwango kikubwa.
















Wanachama wa kikundi cha KIWNET kutoka kaunti ya Kilifi wakikagua baadhi ya stakabadhi zinazoonyesha takwimu kuhusu mimba za mapema katika kaunti ya Kilifi. Kikundi hiki sasa kinaongoza juhudi na kampeini za kumaliza kabisa mimba za mapema katika kaunti hiyo. Picha na Kazungu Samuel

Comments