Monday, August 17, 2009

JAA LA TAKA MWAKIRUNGE:MUNGU TU NDIYE ANAYELINDA WANAOISHI HAPA











Ukifika jaa la taka la Mwakirunge,utakutana na watu wanaoishi kwa taabu ya kuchokora uchafu ndani ya jaa hili.








Lakini kutokana na hali ngumu za maisha nchini Kenya na kuzidi kudorora kwa uchumi wa dunia,watu hawa ndani ya jaa hawana tumaini lolote la kufanikiwa na kile kilichobaki na kuvumilia uvundo na harufu mbaya kuendelea kuishi.








Nilikuwa huko na kunasa baadhi ya picha hizi.Tazama ufanye maamuzi.

SHIDA YA MAJI IMEKUWA DONDA SUGU HUKU KILIFI MKOANI PWANI











Unapopita katika maeneo mengi ya mashambani wilayani Kilifi ni kawaida kuwaona akina mama na watoto wakitembea mwendo mrefu kutafuta maji.








Hali hii imezidishwa na kiangazi cha muda mrefu katika eneo hili ambalo linapakana na mbuga ya wanyama ya Tsavo Mashariki.








Nilipofika huko majuzi,nilikumbana na akina mama wakichimba bwawa ili kutega maji wakati mvua itakaponyesha.Lakini hii pia sio kazi rahisi kama picha hizi zinavyoonyesha.Matatizo kweli ni mengi vijijini.








Tunaweza kuwasaidia wakazi hawa kivipi.




NJAA INAVYOWASUMBUA WAKAZI HUKO KILIFI MKOANI PWANI.





























Hivi majuzi nilizuru maeneo ya mashambani mwa wilaya ya Kilifi katika mkoa wa pwani na kile nilichokumbana nacho kilikuwa dhahiri.Hali hali ya maisha ya wakazi wengi huku inatia hofu kutokana na baa la njaa.














Ingawa serikali inajaribu kuwasaidia kwa kutuma chakula cha msaada,hali haijakuwa na afyeni hivi kwamba wakazi wengi bado wanakodolea macho kifo kutokana na baa hili la njaa.














Kulingana na mahojiano niliyofanya,wengi hawajavuna chochote katika mashamba yao kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita.Na sasa wanataka serikali iwasaidie hata zaidi.














Mwaka wa 2005,taasisi ya kukadiria hali ya umaskini nchini ilizindua ripoti yake ambayo ilionyesha kuwa eneo la Ganze ndilo lenye kiwango kikubwa cha ukata na umaskini uliokithiri.














Tafadhali saidieni wakazi hawa nao wawe na angaa tone la furaha maishani mwao.Picha zinaonyesha hali ilivyokuwa wakati wa kugawanywa kwa chakula hicho cha msaada katika shule ya msingi ya Mnagoni wilayani Bamba.














Kazungu.

Tuesday, August 4, 2009

JUHUDI ZA KUTUNZA MAZINGIRA KATIKA MAENEO KAME NCHINI KENYA.







JUHUDI ZA KUTUNZA MAZINGIRA KATIKA MAENEO KAME.




(Badala ya kuchoma makaa,sasa wakazi washauriwa wafuge kanga na kuuza)

Hivi majuzi,waziri wa mazingira Bw.John Michuki alitangaza mikakati mipya ya kutunza mazingira hasa katika juhudi za uboreshaji wa misitu ya humu nchini ambayo katika siku za hivi karibuni imekuwa walengwa wakuu katika uharibifu wa mazingira unaoendelea katika kima cha kutisha.

Na huku mgogoro kuhusu ukataji miti na shughuli za kilimo ukiendelea kutoa tumbo joto katika msitu wa Mau huko Riftvalley,kampeini za aina yake za kutunza mazingira kwa hivi sasa pia zimeanzishwa katika maeneo kame.

Na kama vile Taifa Leo ilivyogundua ilipokuwa katika eneo la Bachuma Gate huko Voi hivi majuzi,sasa juhudi za kutunza mazingira zimeingiliwa na wakazi wanaotaka kuhakikisha kwamba misitu inalindwa.

Waziri Michuki akiongea hivi majuzi alisema wizara inatayarisha sera ambapo kila mkulima atatikana kutumia asilimia kumi ya shamba lake katika upanzi wa miti.Hii waziri alisema itasaidia pakubwa katika kuhakikisha Kenya inabakia kuwa na mazingira mema baada ya kuona athari za kukatwa kwa msitu wa Mau zikianza kuathiri wakenya.

Katika eneo la Bachuma,Mzee Gerald Macharia mtaalam wa mazingira katika maeneo kame pamoja na Joseph Mburu wameanzisha maradi wa aina yake ambao watarajia kuwa utapunguza kwa kiasi kikubwa shughuli za uchomaji makaa na ukataji kuni katika maeneo haya ambayo ni kame na hupata mvua chache kwa mwaka.

Katika maeneo haya ambayo yanapakana na Samburu,Makina na Maungu,shughuli za ukataji miti zimekuwa zikiendelea kwa kiwango cha kutisha na kutoa taaswira ya kuendelea kwa jangwa katika maeneo haya.

Ni kawaida mtu anapopita katika maeneo haya hasa anaposafiri kwenye barabara kuu itokayo Nairobi kuelekea Mombasa ataona wauzaji makaa kando mwa barabara wakinadi bidhaa hiyo.

Lakini kulingana na Mabw.Macharia na Joseph Mburu,wao wameanzisha kampeini za kuhakikisha kuwa wakazi wanaacha kabisa masuala ya kukata miti na kuchoma makaa badala yake wanawafunza jinsi ya kufuga kanga na kuuzia watalii katika eneo hilo.

Huku wakishirikiana sako kwa bako na shirika la hifadhi ya wanyama pori nchini(KWS) Bw.Mburu na Bw.Macharia wamekuwa wakiingia kutoka kijiji kimoja hadi chengine kuwaelimisha wakazi juu ya mpango huu.”Badala ya wao kukata misitu na kuharibu mazingira,sisi tumeanzisha kampeini za kuwahimiza wafuge kanga na kuwauza kwa watalii na mahoteli katika miji ya Nairobi na Mombasa ambapo wanaweza kupata fedha nyingi na wakaendeleza maisha yao,” akasema Bw.Mburu.

Wakiongea na Taifa Leo katika eneo ambalo wanafugia kanga wengi katika kituo kidogo cha biashara cha Bachuma,mkabala na hoteli ya Tsavo Mashariki,wawili hao walisema kampeini yao imeanza kuzaa matunda kwani baadhi ya wakazi wameanza kuingia mradi huu na pole pole wameamua kuacha kuchoma makaa na wanafuga ndege hawa kwa wingi na kujipatia pato la kila siku.

Katika kituo chao ambacho kimesajiliwa na kutambuliwa na shirika la kuhifadhi wanyama pori(KWS),Macharia na Bw.Mburu wamekuwa wakifuga kanga wengi pamoja na wanyama wengine wa mwitu kama vile sungura.

Katika maeneo kame,maisha huwa ya taabu kwani bayana njaa huonekana kuandama wakazi kila mara.Na kwa kutafuta pesa za haraka,wakazi hukata miti na kuchoma makaa na kuuza kuni katika harakati za kujipatia riziki.

Hiyo ndiyo changamoto ambayo Macharia na Bw.Mburu waliangalia kwa makini na kuona kuwa njia mbadala ya kuhifadhi miti michache iliyopo katika maeneo haya ni kupitia kwa mpango huu.

“Katika nyakati za kwanza hali ilikuwa ngumu na watu wengi walichukulia kimzaha mwito huu lakini walivyoona wanaweza kufuga kanga na kuuza na kupata pesa,sasa wakaamua kujaribu na wengine tayari wameanza kuuza ndege hawa katika hoteli zilizoko katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

Wakati Taifa Leo ikiwasili katika mradi huo wa Game Rescue Foundation,Bw.Mburu na Mzee Macharia walikuwa wamewasili muda mchache kutoka Taru ambapo walikuwa na warsha ya siku moja kuwaelezea wakazi kuhusu mradi huu ambao pindi ukishika kasi,biashara ya makaa na uharibifu mwengine wa misitu itapungua au kumalizika kabisa.

Miezi miwili iliyopita,Bw.Mburu na Macharia walikuwa katika eneo la Maji ya Chumvi ambapo walikuwa na warsha nyengine ya kuwahamisha wakazi waache kuchoma makaa lakini badala yake waanze kufunga kanga ili wauze na kupata mapato.

“Tunafahamu kuwa hali ya maisha katika maeneo kame daima imekuwa ngumu lakini pia tumewaeleza wakazi juu ya mchango mkubwa ambao wanatakikana wawe nao katika kufanikisha mazingira yao,” akasema Bw.Mburu.

Kwenye kituo chao(Sanctuary) wamekuwa wakifuga aina mbili za kanga wajulikanao kama Helmeted guinea fowl na vultureline guinea fowl.”Hawa ndio wanaopatikana katika maeneo kama kama haya lakini kuna ile aina ya kanga aitwaye christened guinea fowl ambaye hupatikana tu katika maeneo yenye misitu mikubwa na baridi kali.

Kulingana na kifungu 376 cha sheria za kuhifadhi na kusimamia wanyama wa pori,kanga wanaruhusiwa kunaswa katika msimu unaoanzia mwezi wa machi hadi mwezi wa novemba.Miezi ambayo KWS inapiga marufuku unasaji wa kanga ni kuanzia mwezi wa desemba hadi feburari.

Kulingana na Bw.Mburu,mradi huu huenda ukawa na faida kubwa kwa wakazi wa Bachuma na viunga vyake kwani mbali na kuwa wakazi sasa wanaanza kupata ajira,hapa sasa kutatumika kama kituo ambapo habari muhimu kuhusu wanyama pori zinaweza kupatikana hasa kwa wasomi na wanasayansi.

“Hiki ni kituo ambacho tunataka kiwe kielelezo kuwa hata katika maeneo kame kama haya juhudi za kuhakikisha mazingira bora na maisha mema zinaweza kuafikiwa,” akasema Mzee Macharia.Kwa sasa wao wana takribani kanga 60 ambao wanafuga na juzi walipata oda inayowahitaji kusafirisha kanga 300 hadi nchini China.

Kutokana na eneo hili kupata mvua chache sana kwa mwaka,wakazi wengi huwa wafugaji ingawa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo njaa isiyo na kikomo.Hali hiyo huwafanya wengi wao kubakia kula matunda ya mwitu kila msimu.

Akiongea na Taifa Leo katika eneo la Makina,mmoja wa wakazi ambao waliamua kuacha kuchoma makaa na badala yake ameanza kufuga kanga Bw.Joseph Mwero alisema anatarajia kuanza maisha mapya katika biashara hii ya kufuga kanga.

”Kwanza biashara yenyewe ilikuwa imeingiliwa na watu wengi hivi kwamba ilikuwa hata kuuza gunia moja la makaa ni tatizo;Lakini tulipoenda kwa semina hii huko Taru,niliamua sitokata tena makaa na badala yake nitajitahidi kufuga ndege hawa kama njia badala ya kuendeleza maisha yangu,” akasema.

Maoni yake yalikuwa sawia na yale ya Justine Mkalla ambaye tulikumbana naye katika eneo la Maji ya Chumvi tukirudi jijini Mombasa.Yeye pia aliniambia kwamba ameamua kuacha mambo ya kuchoma makaa na badala yake ameamua kuanza kufuga ndege hao ili apate kuwauza na kuendeleza maisha yake.

Wakati Taifa Leo ikiondoka katika eneo hilo,sura ya matumaini ilikuwa bayana kwani sasa wakazi wameona mwanga na wanaapa kushirikiana na KWS pamoja na mpango huu ili kuhakikisha pia nao wanapata vibali na kufunga ndege hao ambao huwa na soko kubwa nchini na kimataifa.

MWAMBAO SANAA GROUP KUTOA FILAMU MWEZI HUU


Wasanii wa maigizo kutoka kikundi cha Mwambao Sanaa Group wanatarajiwa kutoa filamu ya kiswahili ambayo inatarajiwa kuwa na ubora wa filamu za kiswahili Afrika Mashariki na Kati.


Filamu hiyo ambayo inajulikana kama DENI ilitungwa na kuelekezwa na mwandishi maarufu wa makala jijini Mombasa Bw.Kazungu Samuel.


Upigaji picha wa filamu hiyo ulifanywa na Justine Katana wa kampuni ya CK Production iliyoko viungani mwa jiji la Mombasa katika mtaa wa Mgongeni-Mwandoni.


Kikundi cha Mwambao Sanaa Group kinapatikana katika eneo la Steji ya Paka huko Bamburi.
Kwenye picha hapo juu,afisa wa uhusiano mwema wa kikundi hicho cha wasanii Bi.Salma Abdalla anaonekana akimpa cheti mwenyekiti wa kikundi hicho Bw.Ludovick Mbogholi pindi tu alipokipata cheti hicho.
Mpiga Picha:Kazungu Samuel

Monday, August 11, 2008

Mwakere asitingisike awe imara

Namuomba waziri Ali chirau Mwakere asibabaike bali awe imara kwani wabunge wenzake wanamuunga mkono.Ukweli ni kwamba viongozi hawa ambao wanasema kuwa bandari ya Mombasa iongozwe na afisa wa kitaifa badala ya mpwani ndio wale wale ambao walisema wanataka mkoa huu wa pwani ujiendeleze na hata wakatoa ajenda nyingi tu ikiwemo suala la Majimbo.Ni jambo la kushangaza kuwa hawakuwa na utaifa huu ambao sasa unajitokeza.Hii ni changamoto kwa wabunge wa pwani kuwa wafanye juu chini na kuongea kwa sauti moja ili bandari hii ya Mombasa ibaki katika himaya ya pwani.

Sunday, August 3, 2008

Mwanajeshi wakati wa mkoloni sasa anauza magazeti Shanzu.




Mzee Mwasi akinieleza kuhusu jinsi alivyokuwa mwanajeshi wakati wa utawala wa ukoloni na pia naibu wa chifu katika eneo la Mbale katika tarafa ya Wundanyi huko Taita.Pia alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu Ronald Gideon Ngala ambaye alikuwa mwanasiasi maarufu katika mkoa huu wa pwani.Pia alikuwa rafiki wa aliyekuwa mbunge wa eneo la Kisauni hapa jijini Mombasa Emanuel Karisa Maitha.Mzee huyu ambaye sasa ana miaka 70 bado ana nguvu za kuuza magazeti katika kitongoji cha Shanzu kwenye barabara kuu ya Mombasa-Malindi.






Ni saa kumi na mbili asubuhi na kituo cha biashara cha Shanzu kimeanza kuwa na utiriri wa shughuli za kuanza siku.Ni jumatatu iliyo na umande kutokana na kijibaridi cha asubuhi.Huu ni msimu wa baridi kali hapa pwani.

Hata hivyo miongoni mwa wakazi hawa wa Shanzu ambao wanaparamia matatu kuelekea katikati mwa jiji kwa shughuli za kikazi,mzee mmoja anaonekana akiuza magazeti katika kioski kilichoko karibu na steji ya pikipiki za bodaboda.

Si rahisi kufahamu chochote kumhusu mzee huyu ambaye anaonekana tuli akiwangoja wateja wafike kibandani mwake kununua magazeti.Lakini uchu wangu wa kutaka kumfahamu mzee huyu unazindua hazina ndefu ya historia iliyojificha kwake.

Sio rahisi kuamini kuwa muuzaji huyu wa magazeti ya Taifa Leo alikuwa wakati fulani mwanajeshi wakati wa utawala wa mkoloni.Fauka ya hayo alikuwa chifu mdogo kabla ya kuwa meneja wa chama kimoja cha ushirika katika sehemu ya Mbale huko Taita.Ni mzee ambaye mazungumzo naye yanakufikisha katika historia ya watu maarufu waliowahi kutawala katika fikra za kizazi cha wapwani miongo iliyopita.

Hata hivyo mbali na historia hii ndefu,Mzee Duncan Julius Mwasi ambaye alizaliwa mwaka wa 1938 katika eneo la Mbale katika tarafa ya Wundanyi alianza kuuza magazeti ya Taifa Leo katika kituo hiki cha biashara mwaka wa 1979.

”Wakati huo kulikuwa na kibanda kimoja pekee katika eneo zima la Shanzu huku sehemu kubwa ikitawaliwa na magugu kando mwa barabara hii.” Akaanza masimulizi yetu katika kibanda chake.

Huku akionekana kufahamu vyema masuala ya biashara hii ya magazeti,Mzee Mwasi alinidokezea kwamba wakati akianza kuuza magazeti haya,bei ya Taifa Leo ilikuwa ni Shilingi moja na senti ishirini pekee(1/20) huku gazeti la Daily Nation likiuzwa wakati huo kwa Shilingi tatu huku lile la Sunday Nation likiuzwa kwa shilingi nne na sumni(4.50).

“Wakati huo kulikuwa hakuna wauzaji wengi wa magazeti lakini kwa sasa vijana pia wameingilia kazi hii katika harakati za kujisukuma kimaisha.” Akasema.

Ni katika mazungumzo yetu ambapo mzee Mwasi alinidokezea kuwa alikuwa rafiki wa dhati wa aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri wa pwani miaka ya sitini marehemu Ronald Gideon Ngala.Urafiki wao ulikuwa mkubwa hivi kwamba mara kwa mara mzee Mwasi alikuwa akilala katika nyumba ya Ngala iliyoko katika mtaa wa Buxton.

“Nikiwa pamoja na marehemu Ngala,mwanawe Noah Katana Ngala ambaye baadaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Ganze alikuwa ni mtoto mdogo pamoja na nduguze wengine.

Mara kwa mara marehemu Ngala alizoea pia kutembelea eneo la Mbale,kijijini kwa mzee Mwasi na kujenga himaya kubwa ya urafiki kati ya familia ya Ngala na ile ya Mzee Mwasi.

Awali mzee huyu alinidokezea kuwa alikuwa mwanajeshi katika serikali ya ukoloni lakini punde tu baada ya Kenya kupata uhuru,mzee Mwasi aliondoka jeshini na kuajiriwa kama naibu wa chifu katika eneo la Mbale.”Nilifurahia mno kuwahudumia wakazi wa Mbale hasa ikikumbukwa kuwa mimi ni mzaliwa wa eneo hilo.” Akasema.

Hata hivyo baada ya kuhudumu kama naibu wa chifu kwa muda mrefu,mzee Mwasi aliamua kujiondoa katika utumishi wa umma na kuzingatia kilimo cha machungwa na mboga katika eneo hilo la Mbale.

Kutokana na ukakamavu wake kibiashara,mzee huyu alichaguliwa kuwa meneja katika chama cha ukuzaji mboga na matunda cha Mbale ambako alihudumu hadi mwaka wa 1979 alipoamua kujiondoa chamani na kuamua kuuza magazeti katika kijiji cha Shanzu.

“Watu walikuwa wakinitaka sana katika chama hicho kutokana na bidii niliyokuwa nayo lakini muda ukafika ambapo niliamua kuacha kazi hiyo kutokana na biashara mbaya iliyosababishwa na ukosefu wa biashara na ushindani uliokithiri.” Akasema

Aliamua kuja katika kijiji cha Shanzu kuanza maisha upya huku akiamua sasa kuuza magazeti.Hata hivyo kutokana na uchache wa wakazi wakati huo,magazeti yote yaliyonuia kuuzwa katika kijiji cha shanzu yaliteremshwa katika jela kuu la Shimo La Tewa na Mzee huyu alikuwa akiyafutata huko.”Nilikuwa nikienda katika jela la Shimo La Tewa ambako magazeti yalikuwa yakishukishwa kabla ya kuyaleta katika eneo la Shanzu.”

Akiwa muuzaji wa magazeti,aliwahi kujenga nyumba na kuwasomesha wanawe kutokana na kazi hii.Mbali na hayo pia aliwahi kuwa karibu na aliyekuwa mbunge wa Kisauni marehemu Karisa Maitha ambaye licha ya kuwa waziri alikuwa akifika kibandani kwake na kupiga gumzo.”Maitha alikuwa ni kama kijana wangu kwa vile alikuwa akija hapa mara kwa mara na kupiga gumzo licha ya kuwa alikuwa waziri katika serikali ya NARC.”

Kabla ya ushindani wa kuuza magazeti kujiri kijijini hapa,Mzee Mwasi alikuwa akiuza magazeti yake katika taasisi mbalimbali kama vile chuo cha walimu cha shanzu,hoteli maarufu ya Serena,jela LA Shimo la Tewa,shule ya msingi ya Shimo la Tewa na hoteli ya Dolphin.

Hadi nikiondoka katika kibanda chake,nilipata taaswira tofauti kumhusu mzee Mwasi na kile kilichojitokeza katika mahojiano naye ni kudhihirika kuwa mzee huyu bado ana bidii ya mchwa na niliondoka huku yeye akisema kuwa bado ataendelea kuuza magazeti haya ya Taifa Leo.