Juhudi za kuboresha utalii wa kinyumbani hapa Kenya(Domestic Tourism)






Wakazi hawa wa jiji la Mombasa juzi walikuwa na kivutio cha aina yake pale kituo kimoja cha utangazaji kilipoandaa tamasha la kukata na shoka ambapo wasanii mbalimbali walitumbuiza.mambo kama haya yanweza kuwa kivutio kikuu cha watalii humu nchini.


UTALII WA NYUMBANI SASA NI KIVUTIO KIKUBWA NCHINI

Utalii wa kinyumbani au kwa kimombo Domestic Tourism ulikuwa ukipuuzwa na wakenya wengi miaka ya nyuma lakini sasa unaendelea kupata umaarufu mkubwa miongoni mwa wakenya.

Nyakati ambako hoteli nyingi zilizoko mwambaoni zilitawalwa na wazungu kutoka mataifa ya Ulaya ikwemo Marekani na Uropa sasa zinaelekea kuisha na badala yake wakenya wenyewe sasa wameamua kuitalii nchi yao ambayo ni bayana imejaaliwa kuwa na mandhari ya kuvutia katika kila pembe.

Kwa mfano katika mkoa wa pwani,kuna mahoteli na fuo za kuvutia ambapo kuanzia Kusini hadi kaskazini,utapata kuna haoteli nyingi ambazo sasa zinatembelewa na wakenya wengi wanaotaka kujivinjari katika mandhari haya.

Na katika enzi hizi ambapo mataifa ya kigeni yakiongozwa na Marekani yamekuwa yakiwekea vikwazo raia wao wasifike nchini,basi imekuwa ni fursa kwa wakenya wenyewe kujivinjari na kuburudika katika fuo hizi za pwani,au kutembelea mbuga za wanyama zilizoko maeneo ya bonde la Ufa au hata vyenzo vingine vya kitalii vinavvyopatikana katika mikoa ya Nyanza na Magharibi.

Ni bayana kuwa mpango huu wa utalii wa nyumbani unapigiwa debe hata na wizara ya utalii ambayo mara kwa mara imekuwa ikiwahimiza wakenya kutalii na kulifahamu vyema taifa lao.

Kutokana na mwito huu mahoteli yamekuwa yakipunguza bei za huduma zao hasa nyakati za watalii wachache na kuwapa wakenya muda mwafaka wa kukodi katika hoteli hizi na kujionea wenyewe mandhari ambayo yanawavutia watalii kutoka Ulaya na Marekani.

Sio hayo tu bali hata ada ya kuingia katika mbuga za wanyama zimekuwa zikipunguzwa katima nyakati fulani ili kuweza kuwapa wakenya muda mwafaka wa kuvinjari na kujionea mandhari ya kuvutia hasa wanyama.

Kulingana na mtandao wa http://www.tembeakenya.co.ke/ ,wizara ya utalii inapanga kuwekeza zaidi katika sekata ya utalii wa nyumbani na kuleta mwamko mpya ya kufufua sekta hii baada ya kuvurugwa awali kutokana na tatizo la ghasia za baada ya uchaguzi.

Kulingana na tovuti hiyo,katibu katika wizara hiyo,Rebecca Nabutola,alisema majuzi kuwa serikali inapanga kuongeza mtaji wake katika sekta ya utalii wa nyumbani kwa kiwango cha asilimia mia moja kama mojwapo ya juhudi za kuweza kuona kuwa sekta hii ya utalii wa kinyumbani inanawiri vyema.

Hali hii inatarajiwa kuwapa matumaini wakenya wengi ambao wamejikuta wakikosa kupata nafasi ya kuvinjari katika mandhari yao ya taifa hili kutokana na gharama kubwa ya kulipia huduma hizi.

Akiongea na Taifa Leo katika ufuo wa bahari wa Pirates,Gabriel Njuguna ambaye ni mkazi wa jijini Nairobi lakini ambaye kwa sasa anajipumzisha katika hoteli moja ufuoni alisema na kukaribisha mwito huo huku akisema utalii wa nyumbani unafaa kulindwa na kuimarishwa zaidi ili wakenya waweze kuingia na vile vile kujumuika katika mikahawa na hoteli za kitalii kwa bei nafuu.

Kuhusu mpango wa wizara ya utalii kuboresha kuwekeza kwa asilimia katika mpango huu wa utalii wa kinyumbani,Njuguna alisema kuwa hilo ni wazo zuri na linalenga kuwapa wakenya ambao wanataka kuingia katika mbunga za wanyama au katika hoteli za kitalii afueni.

Hata hivyo aliitaka wizara ya utalii kusambaza ujumbe wake bayana katika warsha na mikutano mbalimbali katika ngazi za wilaya ili wakenya wengi wapate habari hizi na matukio ya kila siku kuhusu huduma hizi.

”Ingelikuwa bora ikiwa wizara ya utalii itafanya juhudi kubwa za kutangaza utalii wa kinyumbani sio tu katika mikahawa ya kifahari jijini Nairobi bali hata katika ngazi za wilaya ambapo wakenya watajua kile kinachoendelea.” Akasema mfanyibiashara huyo kutoka Nairobi.

Kulingana na wizara ya utalii,baadhi ya huduma ambazo zinalinganishwa na utalii wa nyumbani ni kama vile kuchukua familia na kwenda kujivinjari wakati wa mapumziko,kwenda katika mapumziko ya wikiendi na huduma nyeninge.Haya ni mambo ambayo kimsingi yanafurahisha na ipo haja ya kila mmoja kujitoa mhanga kuhakikisha yana faulu.

Na jiji la Mombasa,utalii huu wa nyumbani sasa umekuwa ukichangamkiwa si haba.Kila inapofika wikiendi,wakazi wa jiji hili huamua kutoka nje ya jiji na kupiga kambi katika ufuo wa bahari wa Pirates/Jomo Kenyatta ambapo hujivinjari huku wakipata upepo mwanana kutoka baharini.

Wengine huamua kufika hapa wakiwa na familia zao na kupanda ngamia,huku wengine wakiogelea na kupanda motaboti za kwenda mbio baharini.Salome Mwikali ni mmoja wa wakazi ambaye awali alikuwa akifanya kazi Nairobi lakini akahamishiwa na kampuni yao hadi eneo hili ambako sasa anafanyia kazi.

Aliniambia kuwa yeye mara kwa mara hufika ufuoni hapa akitalii na wanawe wawili pamoja na bwanake ambaye husaifiri na kuja Mombasa kila wikiendi.”Mimi nikiwa na mzee kila wikiendi hufika hapa kutalii huku watoto wangu wakipanda ngamia na kwenda kujifurahisha.

Bila shaka haya ni mambo ambayo yanavutia na endapo serikali itafanya juhudi kubwa kwa hili,basi tuna matumaini kuwa hata ada ya kulala hoteli hizi za kitalii pia zitapungua na kutupa nasi mwanya wa kuzifikia.” Akasema.

Hivi majuzi akiwa nchini Ujerumani,waziri wa Utalii Bw.Najib Balala aliwahakikishia wageni kuwa taifa la Kenya sasa ni shwari na kwamba lipo njiani ya kuweka mikakati bora kuhakikisha watalii wanaofika Kenya wanapata mandhari ya kuvutia.Juhudi hizi ni kampeini tosha lakini iwapo wageni hawa wanakuwa na tashwishi ya kurudi nchini,ni bayana ipo haja kubwa ya watalii wa humu nchini kuvinjari taifa lao.

Kulingana na mkurugenzi wa bodi ya utalii nchini Dkt.Ongonga Ochieng,utalii humu nchini ulipata pigo baada ya ghasia za baada ya uchaguzi hivi kwamba kunahitajika juhudi kubwa za kuukuza.Katika mazingira ya kawaida,mkurugungezi huyo alisema kuwa Kenya hupata kitita cha Sh.Biliioni moja kutokana na utalii,jambo ambalo linaifanya sekta hii kuwa mojawapo ya sekta ambazo zinahitaji kushuhgulikiwa kwa kina kila inapokumbwa na shida.

Mwenyekiti wa baraza jipya la utalii wa nyumbani(New Domestic Tourism Council Of Kenya) Bi Anastazia Wakesho majuzi alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa baraza lake sasa linajitahidi kuona jinsi utalii wa nyumbani utakavyotumiwa kukuza uchumi wa taifa hili baada ya ghasia za baada ya uchaguzi ambazo ziliwafanya watalii wengi wasifike nchini katima msimu wa mapema mwaka huu.

Baraza hili lenye wanachama 27 lina mipango ambako linatarajia kuongeza kiwango cha utalii wa nyumbani kukidhi na kuafikiana na ule wa nje ili kukabiliana na visa ambapo taifa hili huwa taaban wakati mataifa ya nje yanapokataza raia wao kufika nchini kutokana na sababu moja au nyengine.

Mwaka wa 2006,bodi ya utalii nchini ilirekodi kiwango kikubwa cha mapato kutoka kwa kitengo hiki cha utalii wa nyumbani ambapo kati ya Sh.60.Bilioni ambazo sekta hiyo ya utalii ilipata,Sh.18 Billioni zilitokana na soko la utalii wa nyumbani.

Kutokana na sababu hii wakenya wanamini kuwa sasa utali wa nyumbani ndio jambo ambalo limebaki kwa wizara ya utalii kulipa kipeumbe na kwa ushirikiano na washika dau wengine,wanatumai hali itaimarika katika siku zijazo.

Mwisho.

Comments