Msanii anayeweza kuiga sauti za viongozi na watu mashuhuri Kenya.




Picha hizi zinamuonyesha msanii Mango akiwa anatumubiza katika hafla moja mjini Mombasa hivi majuzi.Yeye anaweza kuiga kwa urahisi sauti za watu.


VIPAJI TELE VYA MCHEKESHAJI MANGO

Unapokutana na msanii Bakari Mango ;( Yeye hudai ni mango lakini sio maembe) akiwa katika harakati zake za kutafuta maisha jijini Mombasa,unaweza kumdhania tu kama yeyote ambaye hana lololte linaloweza kukufanya umuangalie na kumuweka katika fikira zako.

Lakini pindi tu atakapoanza kuigiza sauti ya Rais Mstaafu Daniel Moi na ile ya Waziri Mkuu Raila Odinga,basi hapo ndipo utakapobaini kama uliyeonana naye hasa ni nani.

Karibu katika ulimwengu wa Bakari Mango,msanii ambaye pindi tu unapomkuta viwanjani akitangaza mpira,basi bila kumuona utadhani watagazaji maarufu wa kandanda Ali Salim Manga,Jack Oyoo na Leonard Mambo wamo uwanjani.

Hutasadiki mpaka pale utakapoabaini kuwa yule aliyeshika kipaaza sauti sio mwengine bali ni msanii Bakari Mango.Yeye ni msanii jijini Mombasa ambako amepiga kambi tangu mwaka wa 1985 alipotoka kwao eneo la TransNzoia.

Hivi majuzi nilipata fursa ya kuongea na msanii huyu katika jumba la posta kuu ambako anafanya kazi kama tarishi.

Je Alianzaje mambo haya ya kuigiza sauti hizi za watu mashuhuri kote duniani na jinsi anavyomudu kuongea takribani katika lahaja zote nchini.”Ni mazoea na mimi mwenyewe awali nikiwa katika shule ya msingi ya Mukuyu huko Transnzoia nilizoea kuimba na kughani mashairi na ni hapo ndipo nilipogundua kwamba hata kuongea na kuiga sauti za watu maarufu haikuwa kazi kubwa.” Akasema katika mahojiano yetu.

Msanii huyu majuzi alikuwa miongoni mwa wasanii waliochangamsha mashabiki wa Taifa Leo na wana WAKITA ambao walikuwa wakihudhuria kongamano la kustawisha lugha ya Kiswahili ambayo iliandaliwa na kampuni ya usambazaji habari ya Nation katika hoteli ya kifahari ya Castle Hotel katikati mwa jiji la Mombasa.

Kutokana na umaarufu wake,msanii huyu alituzwa fulani mbili za Taifa Leo na msimamizi wa hafla hiyo Nuhu Bakari.Akiwa mbele ya maafisa wakuu wa Taifa Leo akiwemo meneja wa uhariri Fred Waga na afisa wa usambazaji Harry Njagi,Mango aliweza kuufanya umati uliokuwepo ndani kuvunjika mbavu hasa alipokuwa akimwiga Rais Mstaafu Daniel Moi.

”Nilijisikia mwenye hadhi kwa kupewa nafasi ile katika WAKITA na kudhihirisha jinsi ninavyoweza kueneza talanta yangu katika masuala haya ya sanaa.” Akasema juzi akiregelea matukio ya siku hiyo.”Kwake Mango,usanii una tawala katika damu yake hivi kwamba kila analofanya huwa mwishowe linadhihrisha chembe chembe za usanii.

Kwa mfano hata kazini anakofanyika kazi,mkubwa wake anamfahamu vyema kuwa yeye ni msanii wa vichekesho hivi kwamba mara nyengine huwachekesha hata wafanyikazi wenzake kutokana na anayoyafanya.

”Mimi nataka kila mtu acheke na awe na furaha moyoni;ninachekesha watu nikijua kabisa kuwa mtu anapocheka,sio rahisi kumdhuru mwengine na hili ndilo linaliniteremesha.” Akasema.

Alipokuja jijini Mombasa mwaka wa 1985, aliajiriwa na kampuni ya ulinzi ya KK Guards kama askari lakini pindi tu alipoanza kutumbuiza katika mikutano na hafla za shirika lao,wakuu wake walitambua kipaji alichokuwa nacho na kumpandisha cheo hadi akawa msimamizi wa gari la kubeba walinzi(Crew Commander).

Hili anasema lilimfurahisha mno na kuamini kuwa hata sanaa inaweza kumfanya mtu akatambuliwa kokote nchini na katika nyanja mbali mbali.”Mimi nikiwa KK Guards nilipandishwa cheo kutokana na jinsi nilivyoweza kuwachekesha na kutumbuiza katika mikutano yetu na hali hii yamkini iliwafurahisha wakubwa.” Akasema

Awali alisema kuwa alikuwa akivutiwa sana na wana vitimbi kama vile Mzee Ojwang(Benson WAnjau) na Davis Mwambili(MWala) pamoja na Allan Namisi(Oloibon).Hawa ni wasanii ambao Mango anasema wanajivunia juhudi na talanta zao za kuwa wana vichekesho.

Baada ya kuhudumia shirika la KK Guards kwa muda mrefu hatimaye Mango aliamua kuacha kazi hiyo mwaka jana na kugeukia masuala mengine maishani.Alisema katika mahojiano yetu kuwa kuna nyakati ambazo hatawahi kusahau akiwa katika sanaa hii ya utumbuizaji.

Anataja mfano wa mwaka jana ambako alijikuta akial chakula katika meza moja na aliyekuwa waziri wa vyama vya ushirika Njeru Ndwiga wakati alipokuwa mjini Malindi kufungua tawi la benk ya KITECO.”Watu walishangaa kwa sababu mbali na ulinzi mkali,Ndwiga mwenyewe aliniruhusu nijumuike nao ukumbini baada ya kuwaongoa na kuwaacha watu wote hoi kwa kicheko kutokana na viigizo vyangu.” Akasema.

KWa hivyo inahitaji nini ili mtu aweze kunakili na kuiga sauti za watu bila taabu yoyote.”Kwanza ni sharti uwe na kipawa halafu jambo la pili,ni kuifanya wewe ni yule mtu unayetaka kumuigiza na hapo ndipo utakapofaulu.” Akasema kabla ya kuanza kuigiza sauti ya waziri mkuu Raila Odinga na mgombeaji wa kiti cha Urais Marekani Barack Obama.

Pia Mango amebatizwa jina la Kimaasai akiitwa Lenana.Hii ni kutokana na ukweli wa mambo kuwa jamaa huyu anaweza kuongea kwa lahaja ya kimasaai na ukaamini mtu aliye mbele yako ni Mmasaai kamili.Pia Mango anaweza akaongea kwa lahaja ya Kigiriama,Kikamba,Kikikuyu,Kiluo na kukufanya uamini kuwa yeye ni wa kabila hilo.

Hata hivyo alikiri katika mahojiano yetu kuwa ingawa anajaribu kwa kina kufanya uwezo kamili katika kuigiza lugha za watu,bado anasema sauti ya mtangazaji Leornad Mbotela bado huwa ngumu kwa vile mtangazaji huyo huongeza kwa mkazo mwingi na kumfanya kila anayetaka kumuiga kuwa na kibarua kigumu.”Sauti ya Mambo ni ngumu kuiweka vyema kwa vile yeye kila anapoongea hutumia mkoazo mwingi katika sauti yake na hilo huwa gumu kidogo.”akasema.

Na ni wazi Mango anajivunia usanii huu kwani anasema umempeleka mbali,kuanzia Meru,Maua,Malindi Kilifi na sehemu mblaimbali za pwani.Huku kote amekuwa akifika kutumbuiza.Na wakati wa kampeini za mwaka wa 2007,alikuwa katika msafara uliokuwa ukimpigia debe mbunge wa Kisauni Hassa Joho.”Hata nilipatiwa gari nikawa ninalala nayo nyumbani ili niweze kuwahi katika mikutano hii ya tumbuizo na hili ni jambo ambalo kawme sitahahau.” Akasema.

Vile vile alikuwa miongoni mwa watu waliochangamsha msafara wa naibu waziri mkuu Musali Mudavadi katika uwanja wa Tononoka wakati wa kampeini hizo.”Watu walikuwa wamenyongonyea mkutanoni nami kwa vile nilikuwa karibu nikaomba kipaza sauti na nilipoanza tu kutumbuiza kwa vichekesho vyangu,kila mtu alibaki ameduwaa asijue la kufanya.watu waliburudika.” Akasema.

Kwa sasa anasema usanii huu unaendelea kuwa kwenye damu na anapanga kutafuta wafadhili ili aanze kurekodi video za kazi yake ili auze na kupata mapato.”Unajua kulingana na hali ilivyo,unaweza ukatumbuiza na usibaki na chochote maishani,nia yangu nikutaka kurekodi vichekesho vyangu ili niuze nipate mapato.” Akasema.

Mango Bakari alizaliwa mwaka wa 1972 katika kijiji cha Mukuyu katika sehemu ya Cheranganyi Transnzoia.Alianzia masomo yake katika shule ya maingi ya Mukuyu kabla ya kuelekea katika shule ya upili ya Kitale High.Awali aliwahi kusomea katika eneo la West Pokot lakini akarudi kijijini.Muda huo wote tayari alikuwa akitumbuiza vijijini na sarakasi zake.Ameoa na amejaaliwa watoto watatu,Wasichana wawili na mvulana mmoja.

Mwisho.

Comments