Je muziki wa kizazi kipya utaendelea pwani?







Picha hizi zote zinaonyesha jinsi mambo yalivyokuwa na juhudi za kukuza muziki wa kizazi kipya hapa Mombasa.

Msanii nyota ndogo na Ally B pia ni maarufu mno kwa uchezaji wa muziki wa kizazi kipya.



WIMBI LA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA SASA LAWIKA PWANI

Baada ya muziki wa taarab kuvuma pwani ya Kenya kwa miaka na vikaka,sasa ni dhahiri muda huo umekwisha pwani hii na sasa muziki wa kizazi kipya ndio unaoelekea kutawala katika vilabu na maeneo yote ya burudani.

Ingawa hili linaonekana kuwa jambo geni kwa wazee wa makamu na wale ambao walitazamia muziki wa taarab kuendelea kupata wapenzi wengi kadri miaka ilivyokuwa ikienda,vijana wa kisasa ambao yamkini wanajiita wale wa kizazi kipya wanaendelea kuienzi miziki hii ya kileo na kuipa kwaheri ya kuonana miziki ya taarab.

Kawaida miaka ya sabini na kuendelea hadi miaka ya tisini,hakuna hafla yoyote pwani ambayo ingelifanyika bila kuwepo kwa miziki ya taarab ili kuwaburidisha adnasi kwenye hafla hizo.Lakini leo hii ni bayana kuwa vijana wengi hawana tena musa au hawafahamu tena kuhusu miziki hii na badala yake wanaendeleza miziki ya kizazi kipya.

Miziki hii ni ile ya kufokafoka au maarufu kama Hip-Hop,Salsa,R&B,Genge,Kapuka na Rap.Kwa hilo sasa miziki ya taarab haina afyeni ya kuweza kupenya katika soka la vijana ambao ni idadi kubwa kila wanapovinjari na kujituliza.

Na ili kuonyesha kuwa miziki ya kizazi kipya sasa imegeuka kuwa wimbo jipya la kiburudisho katika mwambao wa pwani,maelfu ya mashabiki walifika hivi majuzi katika ukumbi wa wazi wa Ufuoni katika sehemu ya Jomo Kenyatta kwa onyesho maalum la Famili Fun Show ambalo lilikuwa limeandaliwa na kituo cha Pwani FM pamoja na kampuni ya Kaluworks.

Zaidi ya mashabiki 5,000 walihudhuria tamasha hilo na ilionekana bayana jinsi wanavyoendelea kuufurahia muziki huu ambao kwa sasa umefunika kila aina ya burudani hapa pwani.Na wasanii wengi ili kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya mashabiki wao ambao inaongezeka kila uchao.Jukwaani kulikuwa na zaidi ya wasanii 40 ambao walitoka pembe mbalimbali za mkoa wa pwani kuja na kutumbuiza hapa ufuoni.Kwa mara ya kwanza mashabiki wa miziki hii ya kizazi kipya walijumuika na wasanii ambao yamkini wamekuwa wakiwaona tu katika runinga na kusikia miziki yao katika vituo vya FM ambavyo vimeamua kuwakuza kwa kuwachezea miziki yao kila siku.

Na ili kuzidi kuwainua,vituo vingi hapa pwani navyo vimechukua mkondo mwengine.Awali burudani kubwa ambalo lilikuwa likitawalwa na miziki ya taarab sasa linaendelea kuisha makali huku sasa vipindi kuhusu miziki ya kizazi kipya ikiendelea kunawiri na kuanzishwa katika stesheni za pwani na taifa lote kwa jumla.

Kulingana na DJ maarufu wa Mombasa,Peter Adams ambaye anasimamia kampuni ya Fingerworks DJ na vile vile mtangazaji wa kipindi cha Tafrija kipwani katika stesheni ya Pwani FM,nia hapa ni kujaribu kuwakuza wasanii wa miziki ya kizazi kipya ili nao waweze kujikimu kimaisha kupitia miziki yao.Kwenye mahojiano kadhaa ambayo amekuwa akiyafanya na wanamiziki hawa katika kipindi hiki,DJ huyu anasema kuwa hata hivyo ni sharti kwa wanamiziki hawa wa kizazi kipya wajenge vyanzo vyema na kukita miziki yao katika hatua kubwa ili kuwa na malengo makubwa ya kudumu kama kazi.

”Kimsingi ni kujaribu kuandika mashairi ambayo yatawafaa watu katika maisha yao mbali na burudani,”alisema hivi majuzi akizungumza na wasanii kutoka studio ya kutayarisha muziki ya Greenhouse Records iliyoko Mtopanga.

Vile vile mtangazaji mwengine hapa pwani Bw.Donde Samora pia amekuwa akiandaa kipindi mshindi wa pwani ambapo hupata fursa ya kuhojiana na baadhi ya wasanii wa nyimbo hizi za kizazi kipya na kuona jinsi wanavyoweza kuwafaidi mashabiki wao na vile wao pia kujiendeleza kimaisha kupitia kwa muziki.

Na kutokana na chimbuko hili la miziki hii,basi pia kumekuwa na ongezeko la studio ambazo zinawarekodi wasanii hawa na kuunda midundo ambayo inapokelewa vyema na mashabiki wao;wengi wao wakiwa ni vijana chipukizi.

Baadhi ya studio ambazo sasa zimeanza kujulikana sana ni kama vile Jungle Masters Records ambayo inamilikiwa na msanii maarufu wa Mombasa Prince Adio.Adio aliwahi kuvuma sana kwa kibao chake cha Nikiwa ndani wapiga kelele.Kibao hiki ambacho alikirekodi katika studio ya Tabasam Records kilivuma kama moto jangwani na kwa sasa ameamua kuanzisha studio yake ya Jungle Masters.Ni mmoja wa watayarishaji wa miziki ambao walikuwa katika ufuo huo wa Pirates juzi kuonana ana kwa ana na mashabiki wao na kusikia moja kwa moja jinsi wanavyoenzi miziki yao.

Studio nyengine ambayo pia inajulikana kwa mashabiki wengi ni ile ya Greenhouse Records.Ni studio hii ambayo imewakuza wasanii maarufu wa Mombasa kama vile Nyota Ndgo na Susumila.Nyota ndogo alianzia katika studio hii na kwa sasa amerudi tena katika studio hii akifanya kazi na baadhi ya wasanii ambao alianza nao akiwa hapa.Studio nyengine ambayo kwa sasa imeingiza jinale katika baadhi ya studio zenya mvuto katika mwambao huu ni ile ya Flash Records ambayo ilijulikana baada ya kurekodi kibao cha Kadzo Wangu ambacho kiliimbwa na Ally B.

Studio za zama ambazo bado zinajitahidi kukabiliana na ushindani ni kama vile Tabasamu,Ufuoni,Jikoni na Kelele Records.Pia kuna studio ambazo zinaendelea kuchipuka huku zikiwania soko la muziki huu wa kizazi kipya ambalo ni dhahiri kwa sasa linapanuka pwani.Baadhi ya studio hizi ni kama vile South West Records,Crystal Records,G-Records na G.Stone Records.

Nao wasanii ambao wanaendelea kuvumisha jamvi la muziki huu na kuwafanya mashabiki wao kutoenda kwa muziki wowote mwengine ule ni wengi na walionekana juzi jinsi walivyokuwa wakiwashangilia wasanii hao kila tu walipotaka kuiingia jukwaani kutumbuiza.Baadhi ya wasanii hao ni kama vile Susumila,Escoba,Tasha Family,Mbichwa Family,RP Kelly,na Ruff G ambaye wimbo wake Naja mimi bado unaendelea kushika nambari nzuri katika chati ya pwani.

Na nje ya Mombasa pia kuna wasanii wengi ambao hutetemesha jukwaa kila wanapoingia jukwaani kutumbuiza.Hii ilidhihrika wakati msanii Double S alivyofanya ukumbi wote kupulika kwa kutaka kumuona jinsi alivyokuwa akikatika jukwaani na wimbo wake ukitikisha anga za ufuoni kutokana upigaji mzuri.Kwa dakika tatu ambazo msanii huyu alikuwa akitumbuiza jukwani.Pia msanii Dady S ambaye hurekodia muziki wake katika Studio ya Jungle Masters pia aliwafurahisha mashabiki wake.

Baadhi ya mashabiki ambao Taifa Leo ilizungumza nao walisema wao sasa wameamua kusikiliza miziki ya kizaiz kipya kwa vile hata ujumbe unaotolewa katima nyimbo hizi unahusu maisha ambayo wanaishi kwa sasa.Zile nyakati ambapo vijana tulinyimwa aina ya matumbuizo na kuwaangaliwa wazee pekee wakijifurahisha sasa hamna tena na niwakati wa vijana wenzetu kuongonzana na yote haya ni kupitia nyimbo hizi ambazo tunaimba.” Akasema msanii Susumila.

Kulingana na Jane Akinyi yeye hufurahia muziki wa kizazi kipya si zaidi ila kwa mapigo yake na sauti nyororo za waimbaji chipukizi anaowasikia.”Mimi hufurahia muziki wa kiazi kipya kwa sababu hata magoma yake yamepigwa vizuri tena wasanii wenyewe hata ukiwaona kwenye video wamevaa vizuri na kupendeza,hizi ni nyakati zetu sisi vijana nasi tufurahie.” Akasema.

Naye John Kamau ambaye Taifa Leo ilimpata akijivinjari ufuoni huku akisikiliza kwa makini wasanii wakilishambulia jukwaa alikiri kuwa sasa muziki wa kizazi kipya pwani umeimarika na bado tu mambo kidogo ambayo wasanii hawa wanatakikana kufanya kufikia wenzao wengine wa kitaifa na kimataifa.”Mambo niliyoyaona hapa ni dhahiri kuwa muziki huu wa kizazi kipya hapa mwambaoni umfika mbali na wasanii wana ari ya kujiendeleza kimuziki;hata hivyo ni udhamini tu ndio unaoweza kuwafanya vijana hawa wakapiga hatu kubwa maishani kupitia miziki hii ya kizazi kipya.” Akasema Kamau.


NYOTA NDOGO NA ALLY B WALIVYOCHANGAMSHA UMATI UFUONI

Na KAZUNGU SAMUEL

Kuna msemo usemao kuwa mfalme hatambuliwi kwao.Lakini msemo huu ulikuwa kinyume kwa yeyote ambaye alifika katika tamasha la familia pwani kujionea jinsi wasanii wenye majina makubwa hapa pwani walivyotetemesha jukwaa.

Msanii Nyota Ndogo ambaye anafahamika kote nchini na Ulaya kwa uimbaji wake mwororo na sauti ya ninga alikuwa kivutio cha pekee baada ya msimamizi wa jukwaa hilo Donde Samore kumuita jukwaani kutumbuiza.Pindi tu ilipotangazwa kuwa msanii huyo alikuwa akitaka kuingia jukwaani kutumbuiza,mashabiki wote wakaanza kusukumana kila mtu akitaka kumuona mwanadada huyo ambaye amejaaliwa kipawa kipana cha kuimba.Ilibidi maafisa wa ulinzi kuwa makini na kuzuia baadhi ya mashabiki ambao walisukumana kila mtu akitaka kumshika mkono tu wa Noyta Ndogo.

Naye hakuwavunja moyo kwani kibao chake cha kwanza ulikuwa ni wimbo maarufu sana kote nchini; Ukizaa mwana Shukuru,ukikosa usikufuru.wimbo huu ni miongoni mwa nyimbo ambazo zilimpaisha mno nyota ndogo na kumfikisha pale alipo leo hii.Huku akisaidiwa na bendi ya Love Band,msanii huyu ambaye wengi wanaamini amefaulu kabisa katika miziki hii hapa pwani hakuwavunja moyo bali aliwapa kitu cha uhakika na hivyo basi mashabiki wakakataa aondoke jukwaani.

Baada ya wao kuzidi kukatalia msanii huyu asiondoke,ilibidi nyota ndogo kuwaongezea wimbo kuna watu na viatu.Huu ni wimbo ambao wadau wa miziki na hata vyombo vya habari vimekuwa vikiutaja kama wimbo ambao unaelezea hisia halisi za maisha ya msanii huyu.Na alipomalizia wimbo huu mashabiki wakadinda na kumlazimu msanii huyu kuimba wimbo mpya wa Moto ambao pia kwa sasa upo juu.

Na huku jioni ikiendelea kukaribia,umati uliokuwa hapo ulijipata katika burudani la aina yake baada ya msanii AllyB ambaye anafahmika mno kwa kibao Kadzo wangu alipoalikwa jukwaani kutumbuiza.Hapo msanii huyu alilakikwa na mashabiki huku wengi wao wakiparamia jukwaa na kutaka kumgusa.Ilibidi walinzi katika jukwaa hili kuwazuia na kweli Ally B hakuwavunja moyo kwani aliwaimbia wimbo wake maarufu wa Soldier.Hata hivyo licha ya mashabiki kulilia zaidi,ilibidi AllyB kuondoka jukwaani baada ya kudhihirika kuwa kulikuwa na muda mchache uliobakia.


WAKATAJI VIUNO NAO WALIGEUZA UFUONI KUWA RAHA TELE

Na KAZUNGU SAMUEL

Sio wengi ambao wamewahi kuwqa karibu na wakataji viuno ila tu kuwaona katika runinga au katika picha za video wakifanya kazi yao ya kunengua.Lakini mambo hayakuwa hivyo katika ufuo huu wa Jomo Kenyata huko Bamburi kwani akina dada wa vikundi mbali mbali walijitokeza ukumbini kunengulia baadhi ya waimbaji wa nyimbo za kizazi kipya.

Kuwepo kwa akina dada hawa jukwaani kulionekana kuwa kivutio cha aina yake kwani mashabiki walifurika wakitaka kuwaona jinsi wanavoykata viuno na kuwaacha wengi wao wakiwa hoi huku wakiwataka kutoondoka jukwaani.

Kikundi cha Susumila pia kilikuwa na wanenguaji ambao waliwaacha wengi wakiwa hoi huku mashabiki wakitaka akina dada hao waendelea kuwachezea jukwaani.Lakini ni kikundi hiki cha coastal Dancers ambacho kilionekana kuwavutia wengi kutokana na jinsi kilivyoweza kunengeua kwa ustadi na kuufanya ukumbi kulipuka kwa furaha kuu.

Na kulikuwa na mrembo mmoja ambaye aliamua kujitokeza jukwaani na kunengua katika miondoko ambayo iliwaacha jamaa wakiwa hawana la kusema.Hata hivyo baadhi yao ingawa walikuwa wakifurahishwa na jinsi warembo hao walivyo kuwa wakinengua, lakini baadhi yao walikuwa wamevaa mavazo ya kutatanisha kweli.

Hata hivyo kulingana na Asha Dorothy ambaye pia ni mnenguaji katika ufuo huu,yeye hurufahia kunengua kwa kuvaa nguo hizi fupi kwa vile ndizo zinazotoa mwanya wa mwili kufanya kazi yake.”Hutakikani ucheze huku ukiwa umevaa nguo ambayo inakatiza miondoko yako,ni lazima uvae ile kitu ambayo itakufanya ucheze kwa uzuri zaidi na kupagawisha mashabiki wako.” Akasema msanii huyo.

Baadhi ya waremo mashabiki walisema wao wanafurahia wakataji viuno hao kutokana na kuonyesha kuwa hata wanawake au wasichana wanaweza kunengua na kupata ajira hapa pwani.

”Hii ni kazi na katika kazi yoyote ni lazima ujitume,hakuna litakalokuja kirahisi katika kazi yoyote na ndio unaona ni lazima wasichana hawa wavae hivi ili kurahisisha uchezaji huu.” Akasema Pili Juma ambaye alikuwa miongoni mwa wakazi wa pwani waliofika katika ukumbi huu kutazama au kujiburudisha na tamasha hili.

DARUBINI.

LICHA YA KUJITAHIDI WASANII WENGI HUKOSA UDHAMINI NA KUACHA KUIMBA.

Na KAZUNGU SAMUEL

Licha ya wasanii hapa pwani kujitokeza na kukuza muziki huu wa kizazi kipya,kuna hatari kubwa ya wasanii wengi kupotea na kutosikika tena kwa kukosa udhamini.Mbali na tamasha kama hili ambalo hutokea tu katika majira Fulani,wasanii waimbaji wengi hubaki bila mauzo ya nyimbo zao au chochote cha kujivunia baada ya kukosa udhamini na baada ya muda hukosa kusikika tena.

Baadhi ya wasanii ambao waliongea na Taifa Leo baada ya hafla hii walitaka serikali ifanye juhudi kubwa kuhakikisha kuwa sanaa hii inapalilizwa na kuwa jambo la kujivunia kote nchini.

Wengi walisikitika kuwa baada ya maisha yao katika muziki wakitumbuiza,yamkini hawana ufahamu wa jinsi maisha yao ya mbeleni yatakavyokuwa baada ya kuacha muziki.Na jambo hili walisema husababishwa na kukosa wadhamini ambao wanaweza kupalilia vipaji vyao kwa kuwatafutia soko miziki yao.Mbali na hayo ulegevu wa serikali katika kuhakikisha kuwa kazi hii ya sanaa inatokea kuwa na mapato kwa wanaoifanya pia ni suala nyeti ambalo litanaa kuangaliwa vyema.

”Tunatumbuiza hapa leo na kujivunia mashabiki lakini huwezi kujua baada ya miaka tano utakuwa wapi ikiwa muziki wako hauna mtu wa kukisimamia.” Akasema Escoba.Akiongea Taifa Leo,msanii huyu ambaye alikuwa akiimba na Susumila kabla ya kuachana na kiloa mtu kushika njia yake anasema kuwa udhamini katika muziki ni jambo muhimu ambalo pindi tu lipopuuzwa basi ni sawa na kumtayarishia msanii kaburi lake kimuziki.

Akiongea katika kituo kimoja cha FM hapa pwani,msanii Amani Mele kutoka Malindi na ambaye ana kikundi kiitwacho Snow Family alilalamika kuwa kuna alama tatu za P ambazo zinaposhirikiana vyema msanii anaweza kupiga hatua.Alisema alama hizo ni P ya kwanza ambayo inamaanisha Produsa wa muziki,P ya pili ikiamanisha Presenta(Mtangazaji) na P ya mwisho akiamanisha Promota.”Hawa ni watu watatu muhimu ambao pindi wanapokuwa na ushirikiano mwanana basi wanaweza kupiga kumfanya msanii kupiga hatua kubwa kimaisha kupitia muziki.” Akasema msanii huyo ambaye pia alikuwa ameandamana na mtayarishaji muziki George Okoiti wa G-Stone Records.

Naye msanii Cool Haroun ambaye alivuma na wimbo Machizi akiwa Mombasa kabla ya kuhamia Malindi anakiri kuwa wasanii wengi humu nchini na hasa katika mkoa wa pwani wanakumba na changamoto kubwa kutokana na jinsi hali ilivyo.

Katika taifa la Tanzania,wasanii wengi wanaaminika kupiga hatua baada ya kupata usaidizi kutoka idara Fulani za serikali mbali na kuwa na mapromota wa miziki ambao wamejitoa mhanga kabisa.

Katika Tanzania kuna Baraza La Sanaa Tanzania(BASATA) ambalo nia yake kuu ni kuinua vipaji vya wasanii wa nchini mwao.Na licha ya BASATA kuwa shirika ambalo linapata usaidizi wa kifedha kutoka kwa serikali,baadhi ya wanaolisimamia ni washika dau wenyewe katika sekta ya sanaa nchini Tanzania.Humu nchini bado hakujakuwa na juhudi kubwa za kuwainua wasanii na wengi wao hujibidisha kwa juhudi zao wenyewe ila hufeli kwa kukosa kupata udhamini.

Mwisho.

Comments