SHULE MAARUFU KWA NYIMBO ZA KITAMADUNI.



Wanafunzi wa shule ya msingi ya Uyombo wakitumbuiza wageni katika shule ya msingi ya Matsangoni wilayani Kilifi.Shule hii ilikuwa bora miongoni mwa shule za wilaya ya Kilifi kutokana na uchezaji wake bora wa nyimbo za kienyeji.



SHULE MAARUFU KWA NYIMBO ZA KITAMADUNI: ILIKUWA YA PILI KATIKA MASHINDNAO YA WILAYA HUKO KILIFI: MKOA WA PWANI.

Ni shule ambayo imejificha sana katika lokesheni ya Matsangoni.Sio rahisi kuifikia kwa vile imejificha karibu kabisa na ufuo wa bahari kupakana na Watamu.Hii ndio shule ya msingi ya Uyombo ambayo wengi hawakufahamu ilikuwa na talanta nyingi katika michezo mbalimbali hadi hivi majuzi iliobuka ya pili katika mashindano ya ngazi ya kiwilaya ya nyimbo za kiasili na kwaya.

Mashindano hayo yalifanyika katika ukumbi wa shule ya viziwi ya Kibarani katika viunga vya mji wa Kilifi.Ni hapo ambapo wanafunzi wa kutoka shule hii walipodhihrisha jinsi walivyo na uwezo katika nyimbo za kiasili na kufanikiwa kuibuka wa pili kwa alama 86 nyuma ya shule ya msingi ya Kafuloni kutoka tarafa ya Vitengeni ambayo iliibuka nambari moja kwa alama 86.5.

“Mashindano yalikuwa magumu lakini tulijipanga na kila kitu kikawa bayana kwani ilidhihirika kuwa katika shule ya msingi ya Uyombo,talanta za uimbaji zitele ila ni muda tu kabla ya kuzikuza na kuzifanya kutambulika kitaifa na kimataifa.” akasema mwalimu wa kitengo hicho cha nyimbo za kiasili katika shule hiyo Bw.Mwang’ombe Kalama.

Kutokana na kuibuka nambari mbili katika tamasha hizo za nyimbo wilayani,sasa shule hiyo ya Uyombo ina nafasi ya kusonga mbele katika ngazi ya mashindano ya mkoa.Hata hivyo mwalimu huyo alisema kuwa bado kuna hali ya sintofahamu kuhusu kuendelea kwao na mashindano hayo ya ngazi za mkoa kwani ipo dalili kuwa mashindano hayo yanaendelea na wao hawakuweza kufika.

”Bado hatujajua kama tutaendelea mbele lakini tunangojea kama tutapata barua ya mwaliko kufika katika tamasha za kimkoa ambazi hufanyika jijini Mombasa kila mwaka.” Akasema mwalimu huyo akiongea

Na ilidhirika kuwa shule hiyo imekomaa wakati kikundi hicho cha nyimbo za kiasili kilipotoa burudani ya kuvutia ikitumbuiza katika hafla za kuwatuza wanafunzi waliofanya vyema katika lokesheni ya Matsangoni.

Hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na mkuu wa wilaya ya Kilifi Bw.John Elungata pamoja na mkurugenzi wa elimu wilayani Dickson Ole Keis.Pindi tu kikundi hicho kilipokuwa kikiongoa katika wimbo wake kuhusu mada muhimu ya ugonjwa wa ukimwi.

Katika wimbo wao ambao ulijaa hisia kali,waliimba na kujitupa huku na kule na kwa vile walikuwa wamejichana kwa aina mbalimbali ya mavazi ya kiasili basi ilikuwa rahisi kwa umati hasa viongozi waliokuwepo kujumuika nao na kuaza kucheza na kutoa burudani la aina yake.

Baadaye akiongea na Taifa Leo,mwalimu wa kikundi hicho Bw.Mwangombe alisema kuwa alikianzisha mwanzoni mwa mwaka huu katika shule hiyo ya Uyombo na tayari wamekuwa wakutumbuiza katika hafla mbalimbali katika sehemu hiyo.”Ni mwaka huu ndipo nikishirikiana na bodi ya elimu katika shule ya msingi ya Uyombo ndipo tulipoona ipo haja ya kunasa talanta tele hapa ili kuzitumia vyema na ninashukurua hata wanafunzi wenyewe wamegundua hilo na wanashiriki vyema katika mazoezi haya ya nyimbo za kiasili.” Akasema.

Na kuhusu jinsi walivyocheza mjini Kilifi na kuibuka wa pili,mwalimu huyo aliwashukuru wazazi na walimu wa Uyombo kwa kumtilia mkazo katika kazi yake na vile vile kuwaasa wanafunzi kuhusu umuhimu wa tamasha kama hizi.

”Kila jambo linahitaji ushirikiano na hili ndilo lililokuwa wazo letu tukiingia katika mashindano haya ya tamasha za wilaya na kile kilichijiri kilikuwa cha kutufurahisha mno.” Akasema mwalimu huyo.

Na huku wakiendelea kungojea barua ya kuitwa katika tamasha za ngazi ya mkoa,mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw.Bosco Deche alikuwa akiomba udhamini zaidi ili kuendeleza vipaji hivi vya wanafunzi walio na talanta shuleni.”Sisi katika shule yetu tumebarikiwa kuwa na vijana ambao wana talanta tele lakini tatizo ni ukosefu wa watu wakufuatilia na kunasa talanta hizi na hili tunataka tusaidike ili ndoto zao zifanikiwe.” Akasema.

Iliniajabia kuwa mbali na tamasha hizi za kitamaduni,shule hii ya Uyombo vile vile hutoa wachezaji ambao hufika hata katika ngazi ya kitaifa lakini ambao baadaye hurudi vijijini wakiwa wanahaha kwa kukosa ufadhili.Aidha mwalimu huyo mkuu alisema kuwa mbali na kuwatoa wanamichezo bora katika wilaya ya Kilifi,shule ya msingi ya Uyombo sasa inatawala katika mbio na michezo mingine ya viwanjani huku mwanafunzi wao mmoja akiwa mjini Kisumu kwa mashindano ya kitaifa.

Naye mwenyekiti wa shule hiyo Bw.Wilson Kaboga alisema kuwa nyimbo za asili zina umuhimu katika tamasha kama hizi na akasema wao wataendelea na mipango kabambe ya kuzikuza talanta za wanafunzi hao shuleni humo.

”Hatuwezi kuona vijana hawa wakiwa na talanta tele shuleni mwao lakini badala ya kuzieneza tuwaache tu hilo halitafanyika hapa Uyombo na kwamba mambo mengi yetu ambayo tunafanya tunayatekeleza kwa kuangalia hatima ya wanafunzi wetu pindi tu watakapomaliza shule.” Akasema.

Na huku kikundi hicho kikiondoka jukwaani baada ya kutoa tumbuizo la kukata na shoka,wakubwa waliachwa wakijiuliza,je ni lini talanta kama hizi zitakapoenziwa na kutuzwa kama inavyofanyika katika ngazi za kitaifa na hata kimataifa.

Comments