Mkutano wa WAKITA ulivyofaulu hapa jijini Mombasa.








Hawa ndiyo viongizi wa chama cha WAKITA ambao walichahuliwa katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Royal Castle Hoteli katikati mwa jiji la Mombasa.
Picha ya juu ni mhariri mkuu wa Taifa Leo Fred Waga akiongea na mwenyekiti wa WAKITA Dkt.Abdul Noor.
Katika picha nyengine wanachama wa WAKITA wakisikiza kwa makini hotuba za viongozi wao.
MKUTANO WA WAKITA WAFAULU PWANI
Mkutano wa chama wa wasomaji wa magazeti ya Taifa Leo uliofanyika jijini Mombasa juzi ulifana mno.Mbali na idadi kubwa ya wasomaji na mashabiki wa gazeti ambao walijitokeza katika mkutano huo,iligundulika kuwa kuna vipaji tele vya sanaa na hivi kwamba gazeti la Taifa Leo linatakikana kufanya juhudi kubwa kunasa vipaji hivi. Katika mkutano huo ambao ulifanyika katika hoteli ya kifahari ya Royal Castle Hotel iliyoko katika barabara ya Moi katikati kabisa mwa jiji hili,viongozi wapya walichaguliwa kuendesha jahazi hili la WAKITA. Ni katika mkutano huo ambapo mhariri mkuu wa gazeti la Taifa Leo Bw.Fred Waga pamoja na afisa wa usambazaji Harry Njagi walijumuika ana kwa ana na wasomaji wa magazeti haya. Vile vile mbali na wakuu hao wawili,kampuni ya usambazaji wa habari ya Nation iliwatuma waandishi wao Daniel Muchai,Nuhu Bakari na Douglas Mutua ambao pia walijumuika pamoja na wasomaji.Pia kulikuwa na sherehe mbalimbali ambapo kulikuwa na mashindano ya kutunga na kughani mashairi.Mada kuu ya ambayo wasanii walipaswa kuchangia ilikuwa ni Je mtu kuuitwa mlevi huwa ni sababu gain. Kwenye mashindano hayo,Yusuf Zema ambaye pia hughani mashairi katika kituo kimoja cha FM jijini Mombasa aliibuka mshindi na kutuzwa papo hapo Sh.3,000 pesa taslim.Ali Maingu ambaye pia ni mtangazaji hapa pwani aliibuka wa pili na kutuzwa Sh.2000 pesa taslim. Naye chipukizi Kitsao Samuel Baya ambaye ni mwanafunzi wa mawasiliano katika chuo kimoja jijini Nairobi aliibuka wa tatu na kutuzwa Sh.1,000 pesa taslim.Wote walituzwa mbele ya mashabiki waliofurika ukumbini na afisa wa usambazaji wa magazeti haya Harry Njagi.Vile vile kulikuwa na vichekesho ukumbini kutoka kwa msanii Mango Juma ambaye alimchekesha kila aliyekuwepo ukumbini kwa uwezo wake wa kuiga lugha za watu maarufu nchini na kimataifa. Akiongea baada ya kusikiza maoni ya mashabiki wote waliochangia,mhariri mkuu alisema kuwa baadhi ya kurasa ambazo ziliondolewa baada ya gazeti hili kufanyiwa mabadiliko mwezi wa januari zitashughulikiwa.Alisema kurasa hizi ni kama ule wa makala ya elimu ambao alikiri kuwa umekuwa haba lakini akasema ukurasa huo utarudishwa hivi karibuni. “nimesikiliza maoni yenu kwa makini na kile ninataka kusema ni kuwa yatashuhgulikiwa ingawa baadhi yao yatachukuwa muda kwa vile mpaka yapitishwe katika mikutano yetu;kile ninataka kuwaeleza hapa ni kuwa ule ukurasa wa makala ya elimu utarudishwa kwa vile ulikuwa muhimu sana.” Akasema na kupigiwa makofi. Awali baadhi ya wasomaji walikuwa wamehoji kuhusu kuondolewa kwa ukurasa wa Wanawakita ambao ulikuwa ukiendelezwa kila jumatatu.Mwenyekiti wa WAKITA Dkt Abdul Noor alimtaka mhariri mkuu afanye juhudu kuurudisha ukumbi huo ambapo habari za WAKITA zitakuwa zikichapishwa kila wiki.Awali ukurasa huo ulikuwa ukitumika kila jumatatu lakini muundo mpya wa gazeti ukafanya ukurasa huo uondolewe.Naye Harry Njagi ambaye alielezwa kuhusu shida za kupatikana kwa magazeti ya Taifa Leo katika maeneo ya mashambani aliahidi kuwa magazeti haya sasa yataanza kufika katika maeneo hayo hivi karibuni.Awali wakati wakitoa maoni yao kwa wakuu hawa wa Taifa,baadhi ya wachangiaji walilalama kuwa gazeti hili jipya la Taifa halifiki tena katika maeneo ya mashambani kama ilivyokuwa zamani.Mweka hazinga wa WAKITA Mzee Mohamed Akwabi alitaka gazeti hilo lifike kwa wingi mkoa wa magharibi kwani ni kama umesahaulika. Baada ya hoja hizo,maafisa wapya wa chama cha WAKITA walichaguliwa.Dkt Abdul Noor kutoka Nakuru alihifadhi kiti chake kama mwenyekiti.Mzee Mohamed Akwabi pia alihifadhi kiti chake kama mweka hazina wa WAKITA huku Kinyua Kingori ambaye awali alikuwa katibu mtendaji sasa ni naibu mwenyekiti wa WAKITA.Mshairi wa miaka mingi kutoka pwani Mahmoud Hassan Chatu alichaguliwa katibu mkuu na atasaidiwa na Dennis Otingo. Ali Maingu sasa nfiye katibu mtendaji huku akisaidiwa na Al Amini Somo naye Ann Njeri ambaye ni mkereketwa wa lugha ya Kiswahili akachaguliwa kama kiongozi wa akina mama katika chama cha WAKITA.Ali Khamis Chembea sasa ndiye afisa wa uhusiano mwema katika WAKITA na atasaidiwa na Wanto Warui kutoka Kajiado.Harry Njagi alipitishwa kwa kauli moja na waliohudhuria kuwa mlezi wa WAKITA na mshirikishi wa chama hicho katika kampuni ya usambazaji habari ya Nation. Na akiongea pindi tu baada ya kuchaguliwa tena mwenyekiti,Dkt Noor aliwataka wanachama wote wa WAKITA kuwa kitu kimoja na kuendeleza miradi itakayowafaidi maishani.Alisema kuwa tawi la WAKITA pwani ambalo lilivunjwa miaka mitatu iliyopita baada ya kukumbwa na migogoro ya uongozi litafufuliwa tena hivi karibuni na akawataka mashabiki wa Taifa kujitokeza kujisajili pindi tu tawi hilo litakapofunguliwa tena.”Ninasema hapa kuwa tawi la pwani litaanzishwa tena mwezi ujao na ninawaomba watu wengi wajitokeze pindi tu litakapoanzishwa.” Akasema Vile vile mwenyekiti huyo alisema ufufuzi wa WAKITA pwani baadaye utafuatiwa na ule wa WAKITA Nairobi ambayo sawia ilivunjwa kwa sababu ya malumbano makali.Aliwataka Wakenya waishi kwa amani huku akiwataka wasomaji na wachangiaji wa WAKITA waeneze ujumbe wa amani kupitia kwa maandishi yao.Naye katibu mkuu mpya Hassan Chatu aliwataka mashabiki wote wa Taifa Leo washirikiane naye kwa ajili ya maendeleo chamani.
Mwisho.

Comments