Mwanajeshi wakati wa mkoloni sasa anauza magazeti Shanzu.




Mzee Mwasi akinieleza kuhusu jinsi alivyokuwa mwanajeshi wakati wa utawala wa ukoloni na pia naibu wa chifu katika eneo la Mbale katika tarafa ya Wundanyi huko Taita.Pia alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu Ronald Gideon Ngala ambaye alikuwa mwanasiasi maarufu katika mkoa huu wa pwani.Pia alikuwa rafiki wa aliyekuwa mbunge wa eneo la Kisauni hapa jijini Mombasa Emanuel Karisa Maitha.Mzee huyu ambaye sasa ana miaka 70 bado ana nguvu za kuuza magazeti katika kitongoji cha Shanzu kwenye barabara kuu ya Mombasa-Malindi.






Ni saa kumi na mbili asubuhi na kituo cha biashara cha Shanzu kimeanza kuwa na utiriri wa shughuli za kuanza siku.Ni jumatatu iliyo na umande kutokana na kijibaridi cha asubuhi.Huu ni msimu wa baridi kali hapa pwani.

Hata hivyo miongoni mwa wakazi hawa wa Shanzu ambao wanaparamia matatu kuelekea katikati mwa jiji kwa shughuli za kikazi,mzee mmoja anaonekana akiuza magazeti katika kioski kilichoko karibu na steji ya pikipiki za bodaboda.

Si rahisi kufahamu chochote kumhusu mzee huyu ambaye anaonekana tuli akiwangoja wateja wafike kibandani mwake kununua magazeti.Lakini uchu wangu wa kutaka kumfahamu mzee huyu unazindua hazina ndefu ya historia iliyojificha kwake.

Sio rahisi kuamini kuwa muuzaji huyu wa magazeti ya Taifa Leo alikuwa wakati fulani mwanajeshi wakati wa utawala wa mkoloni.Fauka ya hayo alikuwa chifu mdogo kabla ya kuwa meneja wa chama kimoja cha ushirika katika sehemu ya Mbale huko Taita.Ni mzee ambaye mazungumzo naye yanakufikisha katika historia ya watu maarufu waliowahi kutawala katika fikra za kizazi cha wapwani miongo iliyopita.

Hata hivyo mbali na historia hii ndefu,Mzee Duncan Julius Mwasi ambaye alizaliwa mwaka wa 1938 katika eneo la Mbale katika tarafa ya Wundanyi alianza kuuza magazeti ya Taifa Leo katika kituo hiki cha biashara mwaka wa 1979.

”Wakati huo kulikuwa na kibanda kimoja pekee katika eneo zima la Shanzu huku sehemu kubwa ikitawaliwa na magugu kando mwa barabara hii.” Akaanza masimulizi yetu katika kibanda chake.

Huku akionekana kufahamu vyema masuala ya biashara hii ya magazeti,Mzee Mwasi alinidokezea kwamba wakati akianza kuuza magazeti haya,bei ya Taifa Leo ilikuwa ni Shilingi moja na senti ishirini pekee(1/20) huku gazeti la Daily Nation likiuzwa wakati huo kwa Shilingi tatu huku lile la Sunday Nation likiuzwa kwa shilingi nne na sumni(4.50).

“Wakati huo kulikuwa hakuna wauzaji wengi wa magazeti lakini kwa sasa vijana pia wameingilia kazi hii katika harakati za kujisukuma kimaisha.” Akasema.

Ni katika mazungumzo yetu ambapo mzee Mwasi alinidokezea kuwa alikuwa rafiki wa dhati wa aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri wa pwani miaka ya sitini marehemu Ronald Gideon Ngala.Urafiki wao ulikuwa mkubwa hivi kwamba mara kwa mara mzee Mwasi alikuwa akilala katika nyumba ya Ngala iliyoko katika mtaa wa Buxton.

“Nikiwa pamoja na marehemu Ngala,mwanawe Noah Katana Ngala ambaye baadaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Ganze alikuwa ni mtoto mdogo pamoja na nduguze wengine.

Mara kwa mara marehemu Ngala alizoea pia kutembelea eneo la Mbale,kijijini kwa mzee Mwasi na kujenga himaya kubwa ya urafiki kati ya familia ya Ngala na ile ya Mzee Mwasi.

Awali mzee huyu alinidokezea kuwa alikuwa mwanajeshi katika serikali ya ukoloni lakini punde tu baada ya Kenya kupata uhuru,mzee Mwasi aliondoka jeshini na kuajiriwa kama naibu wa chifu katika eneo la Mbale.”Nilifurahia mno kuwahudumia wakazi wa Mbale hasa ikikumbukwa kuwa mimi ni mzaliwa wa eneo hilo.” Akasema.

Hata hivyo baada ya kuhudumu kama naibu wa chifu kwa muda mrefu,mzee Mwasi aliamua kujiondoa katika utumishi wa umma na kuzingatia kilimo cha machungwa na mboga katika eneo hilo la Mbale.

Kutokana na ukakamavu wake kibiashara,mzee huyu alichaguliwa kuwa meneja katika chama cha ukuzaji mboga na matunda cha Mbale ambako alihudumu hadi mwaka wa 1979 alipoamua kujiondoa chamani na kuamua kuuza magazeti katika kijiji cha Shanzu.

“Watu walikuwa wakinitaka sana katika chama hicho kutokana na bidii niliyokuwa nayo lakini muda ukafika ambapo niliamua kuacha kazi hiyo kutokana na biashara mbaya iliyosababishwa na ukosefu wa biashara na ushindani uliokithiri.” Akasema

Aliamua kuja katika kijiji cha Shanzu kuanza maisha upya huku akiamua sasa kuuza magazeti.Hata hivyo kutokana na uchache wa wakazi wakati huo,magazeti yote yaliyonuia kuuzwa katika kijiji cha shanzu yaliteremshwa katika jela kuu la Shimo La Tewa na Mzee huyu alikuwa akiyafutata huko.”Nilikuwa nikienda katika jela la Shimo La Tewa ambako magazeti yalikuwa yakishukishwa kabla ya kuyaleta katika eneo la Shanzu.”

Akiwa muuzaji wa magazeti,aliwahi kujenga nyumba na kuwasomesha wanawe kutokana na kazi hii.Mbali na hayo pia aliwahi kuwa karibu na aliyekuwa mbunge wa Kisauni marehemu Karisa Maitha ambaye licha ya kuwa waziri alikuwa akifika kibandani kwake na kupiga gumzo.”Maitha alikuwa ni kama kijana wangu kwa vile alikuwa akija hapa mara kwa mara na kupiga gumzo licha ya kuwa alikuwa waziri katika serikali ya NARC.”

Kabla ya ushindani wa kuuza magazeti kujiri kijijini hapa,Mzee Mwasi alikuwa akiuza magazeti yake katika taasisi mbalimbali kama vile chuo cha walimu cha shanzu,hoteli maarufu ya Serena,jela LA Shimo la Tewa,shule ya msingi ya Shimo la Tewa na hoteli ya Dolphin.

Hadi nikiondoka katika kibanda chake,nilipata taaswira tofauti kumhusu mzee Mwasi na kile kilichojitokeza katika mahojiano naye ni kudhihirika kuwa mzee huyu bado ana bidii ya mchwa na niliondoka huku yeye akisema kuwa bado ataendelea kuuza magazeti haya ya Taifa Leo.

Comments